Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Wafanyakazi wa Sekta zote hapa nchini kufanya kazi kwa Weledi na kuwa waadilifu katika utendaji wao kazini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Viongozi, Wafanyakazi na wananchi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Mei Mosi Kitaifa ambayo yamefanyika katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro.
Rais Samia ameyasema hayo Mei 1 mwaka huu wakati akihutubia Viongozi, Wafanyakazi na Wananchi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ambayo Kitaifa yamefanyika katika Uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro.
Viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi nao wameudhuria Maadhimisho ya Sherehe za Mei Mosi Kitaifa ambayo yamefanyika katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro.
Dkt. Samia amesema pamoja na Wafanyakazi hao kudai maslahi yao ya kazi bado wanatakiwa kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa weledi katika kutekeleza majukumu yao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wakiimba wimbo wa mshikamano (Solidarity) kwenye Maadhimisho ya Sherehe za Mei Mosi Kitaifa 2023 katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
“...kwa hiyo pamoja na kudai mishahara bora, lakini uadilifu na weledi kazini ndio utaleta maisha bora kwa wafanyakazi...”. amesema Rais Samia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akigawa zawadi kwa wafanyakazi bora pamoja na washindi wa michezo ya Mei Mosi.
Sambamba na hilo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wafanyakazi kuwa Serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha mazingira ya kazi ikiwemo, kuwapandisha madaraja wafanyakazi, kuwaongezea mishahara na posho za wafanyakazi.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema kutakuwa na nyongeza za mishahara kwa wafanyakazi ambayo itakuwa inaongezeka kwa kila mwaka, nyongeza hiyo inatarajia kuanza mwaka huu 2023.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. FatmaMwassa akiwa kwenye picha ya pamoja Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Morogoro akiwemo Mhe. Sebastian Waryuba Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mhe. Judith Nguli Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Shaka Hamdu Shaka Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Danstan Kyobya, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Mhe. Dkt. Julius Ningu, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame na Mhe. Rebeca Nsemwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa wakati akitoa salam za Mkoa, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa zinazofanywa katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mhe. Fatma Mwassa ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia wafanyakazi Mkoani Morogoro wameboreshewa maslahi yao ikiwemo kupandishwa madaraja takribani wafanyakazi 7108 wamepandishwa madaraja, 2030 wameajiriwa kwa sasa Mkoa umepata kibali cha kuajiri wafanyakazi 3891 wa kada mbalimbali pamoja na kuongeza mishahara.
Nae Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhokya ameishukuru Serikali sikivu ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajali wafanyakazi wake kwa kuwaboreshea mazingira na maslahi yao ya kazi, kulipa2 madai yao, kupandisha vyeo watumishi, pamoja na kuwaongezea mshahara.
Maadhimisho hayo ya Mei Mosi kwa Mwaka huu yanaenda sambamba na kaulimbiu isemayo “Mishahara bora na ajira ni nguzo kwa maendeleo ya wafanyakazi, wakati ni sasa”.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.