Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amebaini sababu za kupungua kwa ufaulu katika shule za Msingi na Sekondari ikiwemo hali ya upatikanaji wa lishe duni hali inayochochea ufaulu kuwa wa wastani Mkoani humo.
Dkt. Mussa amebaini hayo Oktoba 23, Mwaka huu wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea shule za Msingi na Sekondari zilizopo Halmashauri ya Mlimba Wilayani Kilombero yenye lengo la kuangalia hali ya lishe mashuleni.
Akifafanua zaidi, Dkt. Mussa amesema wanafunzi wanaokula chakula cha aina moja hususan makande, ugali na wali bila mboga za majani wala matunda hudumaza afya ya akili na kusababisha ufaulu kushuka darasani.
"... matokeo sio mazuri kwa sababu huku chini hawali vyakula vyenye lishe ambapo wanadumaza afya zao..." amesema Dkt. Mussa Ali Mussa
Kwa sababu hiyo, Katibu Tawala huyo amewataka Maafisa Kilimo wa Halmashauri hiyo kushirikiana na Maafisa Kilimo wa maeneo husika pamoja na Walimu kuotesha vitalu vya mboga mboga kwa kutumia mbolea na mbegu za kisasa ili kupata mboga zitakazotumika wakati wa chakula.
Pia, amewataka walimu kubaini mboga za asili zilizopo maeneo husika zikiwemo mchunga, mbwembwe, mnafu, kisamvu, majani ya kunde na mgagani kuzichuma na kuzikausha ili kuzitumia mashuleni wakati wa kiangazi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Richard Magoma amewashauri walimu pamoja na kamati ya shule kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa shule ili wanafunzi wa madarasa yote kuweza kupata chakula chenye virutubisho vya lishe bora kwani kusubiri hadi madarasa ya mitihani yaani kidato cha pili na cha nne kutaathiri ongezeko la ufaulu mashuleni.
Nae, Afisa Lishe wa Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe amesema walimu pamoja na kamati ya shule inapaswa kubaini namna bora ya kuwashawishi wazazi kuchangia chakula ikiwemo kutoa chakula kinachopatikana katika eneo husika.
Katika hatua nyingine, Afisa Afya wa Mkoa wa Morogoro Bi. Prisca Laurent Gallet amewasisitiza walimu pamoja na kamati za usafi za shule kuhakikisha kunafanyika usafi katika maeneo yote ya shule ukiwemo usafi wa vyoo, kunawa mikono kwa maji tiririka, kuchemsha maji ya kunywa na kutenga vifaa vya kuhifadhia taka hivyo kutasaidia wanafunzi kuepukana na magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa Kipindupindu.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.