Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amevitaka vikundi vya wanawake Mkoani humo kujikita katika shughuli za kiuchumi hasa kilimo biashara kwa kuwa mazao mengi ya biashara na viungo yanaweza kulimwa katika maeneo mengi ya Mkoa huo.
Mhe. Malima amesema hayo Mei 14, Mwaka huu wakati akifunga kikao cha kutambulisha Program ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi inayojulikana kama Imarisha Uchumi na Mama Samia ( IMASA ) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Glonency (nanenane) iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kikiwa na lengo la kutoa elimu ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara Wanawake Mkoani humo.
"... mnatakiwa mtengeze kikundi cha watu kumi au zaidi mpate mbegu za kokoa mpande hadi mvune, mkipata Mil. 20 au 30 mtachagua mgawane au muongeze biashara yenu hapo ni nyie wenyewe..."
Aidha, Mhe. Malima amesema shughuli za kiuchumi hasa Kilimo biashara kinaweza kufanyika katika maeneo mengi ya Mkoa huo ikiwemo Mvomero, Gairo (Nongwe) na Morogoro vijijini (Mvuha) na kubainisha kuwa kilimo kimeongezewa thamani na Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa zao la Kokoa kupanda bei kutoka shilingi 3000 hadi 28000 kwa kila kilo moja.
Katika hatua nyingine, Mhe. Adam Malima amesema kuwapa wananchi fedha haimaanishi umewasaidia kwani uweshezaji wa kiuchumi ni muhimu kutoa pesa na elimu (maarifa) itakayowasaidia wananchi hususan wanawake kuongoza miradi yao na kuweza kufanya miradi yao kwa uhakika zaidi.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi (NEEC) Bibi Being’i Issa amesema biashara ya uwezeshaji ni muhimu kufanya katika vikundi vilivyosajiliwa na Halmashauri na kutumia vikundi hivyo kuboresha biashara zao.
Sambamba na hilo, Katibu huyo amesema mwaka 2023/2024 kuna mipango mahususi ya kuhakikisha kunapatikana wananchi wengi zaidi wenye hali ya chini kuingia katika manunuzi ya uma, hivyo 30% itatakiwa kwenda kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwekezaji kwa wakina mama wawekezaji Mkoa wa Morogoro Bi. Hadija Mbwana amesema wananchi hasa wanawake wamekuwa wakipoteza fursa nyingi kutokana na uhaba wa mitaji hivyo amesema benki zitaimarisha biashara zao kuleta tija kwao, jamii na Taifa kwa jumla.
Ameongeza kwa kuwashauri wanawake hao kuwa wanapaswa kujiunga kwenye vikundi mbalimbali kisha kuungana na kutengeneza viwanda vidogo vidogo ili kutengeneza ajira za kutosha hivyokujikwamua na umaskini.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.