Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ametembelea mabanda na vipando vya nane nane ikiwa ni maandalizi ya sherehe za wakulima na wafugaji maarufu kama Nanenane kwa Kanda ya Mashariki ambazo zinatakiwa kuzinduliwa rasmi Agosti 1 mwaka huu katika viwanja vya Julius Kambarage Nyerere na kuwataka washiriki ambao hawajakamilisha maandalizi hayo wakamilishe kabla au ifikapo Julai 29 mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akiwa pamoja na kamati ya maandalizi ya maonesho ya sherehe za nane nane wakati wakikagua mabanda ya Nane nane, hapa walikuwa banda la Halmashauri ya Mji Ifakara.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Julai 21 mwaka huu wakati akikagua mabanda na vipando hivyo kwa niaba ya Wakuu WA Mikoa mingine ya Kanda ya Mashariki yaani Tanga, Pwani na Dar es Salaam.
Aidha, Mhe. Adam Malima amefurahishwa kuona baaadhi ya Halmashauri zinazoshiriki sherehe hizo zikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Kigamboni kuonekana zimejiandaa vizuri na kutumia nafasi hiyo kuzihimiza Halmashauri ambazo hazijakamilisha maandalizi hayo kukamilisha kabla au ifikapo Julai 29 mwaka huu.
Hapa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima anaangalia aina za mimea ambayo inafaa na isiyofaa kwa malisho ya mifugo.
“...kwa hiyo tarehe 29 tunatarajia kila mmoja awe ameshafanya mambo yake ili tarehe 30 tuanze maonesho ” amesema Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ( wa pili kushoto) akimsikiliza mtaalam kutoka kampuni ya kuzalisha mbolea aina ya minjingu akielezea namna mbolea hiyo inavyofanya kazi kwa aina mbalimbali za mazao.
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima amesema Kanda ya Mashariki imekuwa mara zote inafanya vizuri katika maonesho ya Nane nane hivyo amewataka wadau wote wa Kanda ya Mashariki kuendeleza sifa hiyo ya kufanya vizuri.
Hapa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam Malima anaangalia ufugaji wa samaki kwenye banda la Halmashauri ya Manispaa Kigamboni.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Dkt. Rozalia Rwegasira amesema zaidi ya Taasisi 500 watashiriki katika Maonesho ya mwaka huu ambayo ni sawa na asilimia mia moja ukilinganisha na maonesho ya mwaka jana ambapo wadau au Taasisi 400 pekee walishiriki.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima (katikati) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa (kushoto) kulia ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na uzalishaji Dkt. Rozalia Rwegasira wakati wakikagua mabanda ya Nane nane.
Aidha, Dkt. Rozalia ameongeza kuwa katika maonesho ya mwaka huu wakulima watajifunza teknolojia ya malisho ya mifugo kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya wafugaji kukosa malisho ya mifugo wao pamoja na kupata Elimu Bora ya kilimo cha viungo kama Karafuu Pilipili Manga na mdarasini.
Maonesho ya Nane nane 2023 ni maonesho ya 30 tangu kuanzishwa kwake huku kauli mbiu ikiwa ni ”Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula”.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.