Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa ushirikiano walioutoa kipindi cha kabla, wakati na baada ya zoezi la uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka huu ambapo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili cha awamu ya sita.
Mhe. Adam Malima ametoa shukrani hizo leo Novemba 4, 2025 Ofisini kwake wakati akiongea Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro Dkt. George A. Pindua alipofika ofisini kwake kuzungumzia ratiba za uapisho wa Askofu huyo Mteule ambazo zilikuwa zifanyike tar. 9 Novemba, 2025 hapa Mkoani Morogoro.
Mhe. Adam Malima amesema katika suala nzima la utulivu, Amani na Usalama uliopatikana ndani ya Mkoa wa Morogoro kabla ya zoezi la upigaji kura, wakati na baada ya wananchi kupiga kura, si la mtu mmoja anayestahili kupongezwa bali pongezi hizo ni za watu wote na wakazi wote wa Mkoa wa Morogoro.
Aidha, Mhe. Adam Kighoma Malima amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kudhibiti hali ya Ulinzi na Usalama ndani ya nchi kwa kipindi chote cha zoezi hilo na kuwezesha leo watanzania kurejea katika shughuli zao za kawaida za kiuchumi na kijamii.
Akipokea pongezi kutoka kwa Askofu Mteule wa KKKT Dkt. George Pindua kwa kuuweka Mkoa katika hali ya Utulivu na Amani, Mhe. Malima ametumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa Viongozi wote wa Dini na madhehebu mengine walioko ndani ya Mkoa huo kwa ushirikiano na kazi kubwa waliyoifanya ya kuhubiri Amani, Upendo na Utulivu na kumwomba afikishe salam hizo za shukrani kwa viongozi wenzake wa Dini wa Mkoa huo.
Pia shukrani hizo amezipeleka kwa makundi mbalimbali wakiwemo wazee akinababa,Vijana, wafanya biashara, wakulima na wafugaji pamoja na wanahabari ambao wote kwa pamoja wamefanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii si juu ya umuhim wa kupiga kura tu bali pia kupiga kura kwa Amani na utulivu.
Mkuu wa Mkoa hakuyasahau makundi ya mama lishe, baba lishe, machifu wa maeneo mbalimbali ya Morogoro, wamachinga, Asasi zisizo za Kiserikali, bodaboda madereva wa magari makubwa ya mizigo, mabasi, madereva wa daladala na bajaji na wote ambao hajawataja bila kukusudia lakini nao amewataka wapokee pongezi hizo.
Amesema, makundi hayo yote yamechangia kwa kiasi kikubwa katika kuuweka Mkoa huo katika hali ya utulivu ambapo hadi sasa upo shwari na wananchi wake wanaendelea na kazi zao za kila siku kwa amani na utulivu. Na kuendelea kuabudu katika nyumba zao za ibada bila mashaka.
Hata hivyo pongezi za shukrani amezielekeza kwa Kamati yake ya Ulinzi na Usala ya Mkoa, KUU Wilaya Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Vijiji/Mita na watumishi wote wa Umma ndani ya Mkoa huo na Taasisi zote za Serikali.
Naye Askofu huyo Mteule wa KKKT Dayosisi ya Morogoro amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano anaouonesha tangu alipoanza kuuongoza Mkoa wa Morogoro lakini pia kwa kipindi hiki cha maandalizi ya zoezi la kupiga kura ambapo aliwaalika katika vikao mbalimbali vilivyohusu mstakabali wa upigaji kura na kwamba hiyo ndio imechangia sana kuleta utulivu. Wa mkoa.
Katika hatua nyingine mazungumzo ya Mkuu wa Mkoa Adam Kighoma Malina na Askofu Mteule George Pindua yalihusu KUAHIRISHWA KWA IBADA YA KUINGIZWA KAZINI KWA ASKOFU MTEULE DKT. GEORGE A. PINDUA PAMOJA NA MSAIDIZI WAKE MCH. PETER MICHAEL MAKALLA.
Hafla hiyo ya Kuingizwa kazini Askofu Dkt. George Pindua iliyopangwa kufanyika Tarehe 9 Novemba, 2025, kwa sababu zisizozuilika imeahirishwa hadi tarehe 14 Disemba, 2025.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.