Serikali Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro imewataka wananchi wanaoishi mabondeni kuhamia katika maeneo maalumu yaliyotengwa na Halmashauri hiyo ili kuepukana na athari za maafa ya mafuriko.
Hayo yamebainishwa Mei 18, 2021 Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro na Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Adam Mgoyi wakati wa ufunguzi wa semina ya siku tatu ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu maafa yatokanayo na mafuriko.
‘’Natoa wito kwa wananchi wanaojenga katika mapito ya maji wanazuia maji kufuata mkondo wake na kusababisha maafa ya mafuriko, lakini pia wa mabondeni wahamie maeneo ya miinuko, waliojenga kwenye maeneo ya kilimo na waliogeuza maeneo ya kilimo kuwa makazi baadala ya kujenga makambi ya muda kwa ajili ya kusimamia mashamba yao warudi katika maeneo tuliyowapatia’’ amesema Mgoyi
Mgoyi amebainisha kuwa kumekuwepo na utamaduni wa wananchi kutaka fidia maafa yanapotokea bila kutambua wao ni sehemu ya visababishi vya maafa hayo huku akiwasistiza kutokuwepo fidia kwa mwananchi ambaye atakaidi maagizo ya Serikali.
Sambamba na hayo, amefafanua kuwa Serikali Wilayani humo imeanza mpango mkakati wa kuhuisha miundombinu ya maji ili kusaidia kukabiliana na kasi ya maji ambayo inaleta athari kwa wananchi Wilayani humo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu Kituo cha Oparesheni Mawasiliano ya Dharura, Ndg. Selestine Masalamado, amewataka wananchi Wilayani humo kuchukua hatua za kupunguza athari za maafa zikiwemo kutochimba madini kando ya mito, kutofanya shughuli za kilimo na ufugaji kando ya mito hiyo.
Naye Katibu Tawala Msaidizi (Mipango na Uratibu) ambaye pia ni Mratibu wa Usimamizi wa maafa Mkoa wa Morogoro, Anza Ndossa amebainisha kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa wananchi hao kwa kuwa Wilaya ya Kilosa ina kata 40 huku 11 kati ya hizo zinaathirika na mafuriko ambapo kijiji cha Kitete huathiriwa sana na maafa, ambapo Machi 2020 kaya takribani kaya 791 ziliathirika kwa maafa ya mafuriko.
Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamaji (IOM), Reuben Mbugi ameihakikishia Serikali yaTanzania kuwa wataendelea kushirikiana nao katika kuijengea jamii uwezo wa kukabiliana na maafa yatokanayo na mafuriko.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Kichangani, Tindiga na Changarawe wameishukuru serikali kwa kuendesha elimu hiyo ambayo itawasaidia katika kujenga uwezo wa kujiandaa, kuzuia na kukabili maafa ya mafuriko iwapo yatatokea.
Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Uratibu wa Maafa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Kilosa chini ya Ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamaji (IOM), wanatoa Elimu kwa Umma inayolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu maafa yatokanayo na mafuriko katika kata tano za wilaya hiyo zilizo katika hatari zaidi ya kuathirika na maaafa ya mafuriko.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.