Waziri Mkuu mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda amevitaka vikundi mbalimbali vya Vijana, akina mama na makundi maalum kuchukua mikopo ya asilimia 10 ili kuongeza mitaji hivyo kuwa na uzalishaji wenye tija.
Mhe. Mizengo amesema hayo Agosti 8, mwaka huu wakati wa kilele cha maonesho ya siku ya wakulima maarufu kama Nanenane kanda ya mashariki yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro yakiwa na lengo la kutoa elimu na kuwajengea uwezo wakulima, wafugaji na wavuvi.
Waziri Mkuu Mstaafu huyo amebainisha vikundi hivyo kuwa ni vile vinavyojihusisha na kilimo,ufugaji na uvuvi kuchukua mikopo hiyo ili kuongeza mitaji yao na kuzalisha kwa tija.
"... tumevikuta vikundi viko hali ya juu kiuchumi lakini vimetokana na mfuko wa 10% na vingine vinapaswa kuchukua kutekeleza majukumu yao, Wakurugenzi wa Halmashauri waliangalie hilo..." Amesema Mhe. Peter Pinda
Akifafanua zaidi, Mhe. Pinda amesema Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri wanatakiwa kuibua vikundi vitakavyonufaika kutokana na mikopo hiyo ili kuendana na kasi ya kiteknolojia katika uzalishaji wa mazao ya Kilimo, ufugaji na uvuvi.
Aidha, Mhe. Pinda amesema kilimo, ufugaji na uvuvi umesaidia kupunguza tatizo la ajira hapa nchini kwani vijana wamekuwa wakifanya shughuli hizo kama vyanzo vikubwa vya kuwaingizia kipato.
Waziri Mkuu huyo mstaafu amehimiza umoja na mshikamano ndani ya kanda hiyo kwani ina rasilimali watu zaidi ya Mil. 13 sawa na 21.4% ambapo Dar es salaam ina watu Mil. 5, Morogoro ina watu Mil. 3, Pwani ina watu Mil. 2 na Tanga - mil 2.6 ambao ndio chanzo cha uzalishaji mali katika shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mizengo Pinda amewataka wananchi kula mlo kamili hususan vyakula vya aina ya mboga mboga kuepuka matatizo ya kiafya ukiwemo ugojwa wa utapia mlo ambao husababishwa na kula vyakula bila kujali lishe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika ushiriki wa maonesho ya Nane Nane kanda ya mashariki 2024 kutokana na kuwepo kwa ubunifu wa kiteknolojia katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi, ambapo yamefanya maonesho hayo kuvutia zaidi hapa nchini.
Pia Mhe. Malima amesema Kanda hiyo inapaswa kutumia fursa ya ardhi iliyopo kwa ustadi ili kujipatia chakula cha kutosha, huku akihimiza maonesho hayo kuwa ya vitendo zaidi kwa kile kinachooneshwa na wataalam ndani ya viwanja vya Nanenane vikafanyike maeneo wanakofanyia kazi.
Hata hivyo, Mkuu huyo amewataka wafugaji na wakulima kuwa mfano hapa nchini, kuishi kwa amani na kuheshimiana na kuwataka wafugaji kuwa na maeneo yao ya kulishia mifugo ili kuondoa migogoro isiyo kuwa na tija hapa nchini.
Maonesho ya nanenane hufanyika kila mwaka kuanzia Agosti 1 hadi 8 ambapo mwaka huu yamekuwa na kaulimbiu inayosema " Chagua viongozi bora wa Serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, mifugo na uvuvi"
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.