Ujenzi wa miundombinu bora ya barabara na daraja la luipa imewasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa vijiji vya misegese, Chiwachiwa na Lavena vilivyopo kata za Namawala na Mbingu Halmashauri ya Mlimba na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na mazao kwa urahisi.
Hayo yamebainishwa Aprili 16, 2025 na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ndugu Ismail Ali Ussi wakati akifungua daraja hilo katika kijiji cha misegese ambalo limegharimu zaidi ya Tsh. Bil. 1.9.
Aidha, Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge kitaifa amesema hapo mwanzo daraja la Luipa lilikuwa kikwazo kwa wananchi katika kusafiri na kusafirisha bidhaa mbalimbali kwa sasa kero hiyo imekwisha baada ya daraja hilo kujengwa na kukamilika chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suhulu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"...daraja hili lilikuwa changamoto kwa wananchi wetu kutoka eneo moja kwenda jingine lakini kwa mapenzi aliyonayo Rais Samia leo hii tunajionea daraja la kisasa na shughuli zetu za maendeleo tunaweza kufanya muda wowote..." amesema Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge
Sambamba na hayo ndugu Ismail amewataka wananchi kutunza na kuthamini miradi ya maendeleo ambayo serikali inayotumia fedha nyingi kuibuni na kujenga ili kukuza uchumi wa jamii na nchi kwa ujumla hivyo jamii inapaswa kuitunza na kuendelea kutumika vizazi na vizazi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mlimba Mhe. Godwin Kunambi amesema mbali na daraja hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suhulu Hassan ameazimia kujenga madaraja mengine sita ya kiwango cha juu katika vijiji vya Chiwachiwa, Isago, Mpanga, Mfuji na Mbasa ili kuboresha miundombinu ambayo ndio chachu ya maendeleo.
Awali akitoa taarifa ya daraja hilo, Mhandisi Nurdin Msengi kwa niaba ya Meneja wa Wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) Wilaya ya Kilombero amesema mradi huo umerahisisha wananchi kufika maeneo ya huduma za Kijamii na Kiuchumi kwa wakati hususani wakati wa masika na kutumika kama barabara ya kimkakati ya kukuza uchumi wa Halmashauri ya Mlimba Wilayani kilombero ili kuwa kitovu cha mapato kwa manufaa ya Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.