Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, amewasisitiza walezi wa vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalum Mkoani Morogoro kuwalea watoto hao kwa misingi yenye maadili mema na yanayompendeza Mungu, ili kuwa na kizazi bora cha baadae.
Mhe. Shaka amesema hayo wakati akikabidhi zawadi za Eid Al-Fitr, kwa watoto wa vituo vinne vya kulelea watoto wenye mahitaji maalum vya Mkoani Morogoro akimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima, zawadi ambazo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusisitiza kuwa maadili ndiyo nguzo kuu ya kudumisha amani na utulivu hapa nchini.
Mkuu huyo wa wilaya amesema, ni jukumu la walimu na walezi kuwalea watoto hao katika maadili mema, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya mazingira yao hususan ya shule na vituo vya malezi, ili watoto hao wapate elimu itakayowawezesha kujitegemea kiuchumi kwa siku za usoni.
"Endeleeni kuwalea watoto hawa kwa misingi inayompendeza Mwenyezi Mungu ili tuwe na kizazi bora cha baadaye," amesisitiza Mhe. Shaka.
Aidha, Mhe. Shaka ameihimiza jamii kutambua kuwa jukumu la kuwalea watoto yatima, wenye mahitaji maalum na wanaotoka katika mazingira hatarishi si jukumu la walezi wa vituo hivyo pekee au la serikali, bali ni la jamii nzima.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Morogoro, Bi. Amisa Amir Kagambo, amesema jumla ya vituo vinne vya makao ya waoto wenye mahitaji maalum na cha kituo kimoja cha kurekebisha tabia (Geleza la wafungwa Kilosa) vimetembelewa huku akiweka bayana kuwa zaidi ya watoto 300 wameguswa na mkono wa Eid na kutumia fursa hiyo kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kusimamia zoezi hilo hadi kufanikiwa.
Naye Shekhe wa Wilaya ya Kilosa, Bw. Nasoro Mirambo, alimshukuru Rais Samia kwa kuwakumbuka watoto hao wenye uhitaji, akisema kuwa kitendo hicho ni faraja kubwa kwao, kwa wazazi wao, ndugu na hata kwa jamii nzima.
Baadhi ya watoto waliopokea zawadi hizo waliiomba jamii iendelee kuwakumbuka na kuwasaidia. Miongoni mwa watoto waliotoa shukrani na maombi hayo ni pamoja na Brayton Adi, alimshukuru Mhe. Rais kwa zawadi alizowapati akisema, "Mhe. Rais siyo tu kiongozi wa nchi, bali pia ni mlezi wao.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.