Shilingi Bilioni 9.3 zimetengwa Mkoani Morogro kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji 67 ambayo ipo vijijini na itatekelezwa ndani ya mwaka wa fedha 2020/2021.
Hayo yamebainisha Januari 15 mwaka huu na Mkurugenzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi John Msengi katika kikao kazi cha wadau wa maji Mkoani Morogoro kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Morogoro Hotel.
Mkurugenzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi John Msengi akisikiliza maoni ya wadau kuhusiana na Kikao hicho.
Mhandisi Msengi amebainisha kuwa hadi Disemba 2020 huduma ya maji katika Mkoa wa Morogoro ilifikia asilimia 69 Vijijini na maeneo ya Mijini asilima 81ambapo lengo kubwa la kikao hicho lilikuwa ni kushirikishana mipango katika kuhakikisha huduma ya maji katika Mkoa huo inafikia asilimia 85 Vijijini na asilimia 95 Mijini kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi – CCM ya mwaka 2020/2025.
Aidha, Mhandisi Msengi amesema katika miradi hiyo 67 inayotarajiwa kutekelezwa Mkoani humo italeta mapinduzi katika sekta ya maji ambapo atashirikiana na Wahe. Wabunge kuhakikisha kila kijiji kinapata huduma ya maji safi na salama ndani ya miaka mitatu ijayo.
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya walioshirikiki katika Kikao kazi cha wadau wa maji Mkoani Morogoro, wa kwanza ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi, wa pili ni Siriel Mchembe Mkuu wa Wilaya ya Gairo
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maji, Mhandisi Msangi amesema kutokuwepo kwa fedha za kutosha kukidhi gharama za uendeshaji wa miradi hiyo na uharibifu wa vyanzo vya maji unaopelekea vyanzo hivyo kukauka ni changamoto kubwa inayojitokeza katika Mkoa huo.
Kwa upande wake Mgeni rasmi wa Kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare, amesema hali ya upatikanaji maji safi na salama Mkoani humo kwa takwimu za Disemba 2020 kuna ongezeko la asilimia 13 kutoka asilimia 56 kwa mwaka 2015 ambapo kwa Manispaa ya Morogoro upatikanaji wa maji hayo imefika asilimia 81.
Wabunge kutoka Majimbo tofauti Mkoani Morogoro ambao wamehudhuria kikao kazi cha maji Mkoani Morogoro, kushoto ni Mhe. Abubar Asenga (Kilombero) kushoto kwake ni Mhe. Dennis Londo (Mikumi), anayefuata ni Mhe. Innocent Kalogelesi (Morogoro Kusaini) na Mhe. Tale Tale (Morogoro Kusini Mashariki)
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wahe, Wabunge kutoka Mkoani Morogoro akiwemo Mbunge wa Jimbo la Kilombero Abubakar Asenga amesema jimbo lake linakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji kutokana na jimbo hilo kuongezewa kata kumi hivyo kufikia jumla ya kata 19.
Pia, amesema katika Jimbo lake kuna mradi wa maji mserereko wa zaidi ya shilingi bilioni sita ambao unatarajiwa kuhudumia wananchi 125,000 kutokana na takwimu za mwaka 2020.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mikumi Denis Londo, amesema licha ya maji kuwa changammoto katika Jimbo lake kuna mradi wa maji wa Madibila ambao ushafanyiwa kazi, kilichobaki ni kupata fedha zitakazowezesha kupata maji ya mserereko kutoka chanzo hicho ambacho kitaondoa changamoto ya maji katika Tarafa ya Mikumi.
Mwenyekiti wa CCM Halmashauri ya Wilaya ya kilosa Ndg. Amer Mubarak amesema kuna mwingiliano mkubwa wa kazi baina ya MORUWASA na RUWASA hali inayopelekea mamlaka hizo kushindwa kutekeleza wajibu wao inavyotakiwa, hivyo ameiomba Serikali iingilie Kati kutatua changamoto hiyo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.