JUMUIYA ya Kiislamu ya Ahmadiyya Morogoro imetoa msaada wa zaidi ya Kaya 110 zenye uhitaji zilizopo Kata ya Kihonda Maghorofani Manispaa ya Morogoro ikiwa ni chakula kwa ajili ya Mkono wa Eid Fitri ambapo utaratibu huo umekuwa ukifanyika kabla ya Sikukuu.
Hafla hiyo fupi ya ugawaji wa vyakula imefanyika Mei 09/2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ahmadya Kihonda Maghorofani.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo la ugawaji wa vyakula, DC Msando, ameomba mashirika na Taasisi zingine yakiwemo madhehebu ya dini kuelekeza misaada mbalimbali kwa wananchi wenye uhitaji maalumu ili kutengeneza furaha na kudumisha umoja baina yao na wenye uhitaji.
DC Msando,ambaye ndiye mgeni rasmi wa hafla hiyo fupi ya ugawaji wa chakula kwa wenye mahitaji akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martine Shigela, amesema Ahmadiyya wamefanya jambo la Uchamungu ambalo linatakiwa liigwe na Taasisi nyengine.
Naye Mkuu wa Chuo cha Jumuiya ya Ahmadiyya Morogoro, Sheikh Abid Mahmood Bhatti, amesema kuwa msaada huo umetolewa kuunga mkono wito wa Serikali inayohimiza mashirika, taasisi, na watu binafsi kutoa misaada kwa jamii yenye uhitaji.
Bhatti, amesema licha ya kuunga mkono Serikali lakini pia kuweza kutoa zakatul Fitri kwa jamii ili kuweza kujumuika na jamii katika kusherehekea Sikukuu ya Eid Fitr ambayo tayari imeshapita japo wamekuwa wakifanya kabla ya Sikukuu.
"Jumuiya ya Ahmadiyya ni moja ya sehemu inayojihusisha na utoaji wa misaada mbalimbali ikiwemo ya kiafya,kielimu na kijamii kwa kuwafikia watu wenye uhitaji, hivyo kutoa kwetu chakula kwa watu wenye uhitaji kwanza tumetekeleza misingi ya dini , kwani sisi tumekuwa tukifanya hivi kila ifikapo Siku ya Eid basi tumekuwa tukijumuika na ndugu zetu kuhakikisha kwamba tunakuwa nao pamoja katika kusheherekea sikukuu hii." Amesema Bhatti.
Miongoni wa vyakula hivyo vilivyo gharimu takribani Shilingi Milioni 2 na laki 5, ni pamoja na Mchele mfuko wenye Kilo 5 na Unga wa Sembe Mfuko wa Kilo 10 kwa kila Kaya.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.