KASI YA MAENDELEO NI KUBWA REA NA TANESCO FANYENI KAZI - DKT. BITEKO.
Naibu Waziri Mkuu ambae pia ni Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko (MB) amezitaka Mamlaka ya Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) na Shirika la Usamabazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuendana uhalisia wa uhitaji wa nishati ya umeme na kasi ya maendeleo hapa nchini.
Dkt. Doto Biteko amesema hayo Mei 31, 2024 wakati akifungua rasmi kituo cha kupoza umeme cha Ifakara Mji kilichopo Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro huku akibainisha kuwa mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 24.59 huku shilingi bilioni 18 ni ufadhili wa jumuiya ya Ulaya kupitia mfuko wa maendeleo wa umoja wa Jumuiya ya Ulaya ( European Development Fund EDF).
".... TANESCO na REA endeleeni kuwahudumia wananchi kwa sababu kasi ya maendeleo ni kubwa sana .." amesema Dkt. Biteko.
Aidha Dkt. Biteko amesema mradi huo utaenda kuongeza thamani ya mazao yanayochakatwa kupitia viwanda kama mchele huku wakitarajia kufungua viwanda 54 vitakavyotumia umeme na pia umeme huo utatumika mashuleni ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Hata hivyo Dkt. Biteko amesema kuna uhitaji wa kufungua Ofisi ndogo katika maeneo ya karibu na kituo hicho ili kuweza kusogeza zaidi huduma hiyo kwa wananchi huku akiwapongeza wakandarasi waliotekeleza ujenzi wa kituo hicho akisema wamefanya kazi nzuri na kuutendea haki mradi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa wa Morogoro ndio Mkoa unaongoza kwa uzalishaji wa sukari Nchini hivyo kupitia mradi huo utakwenda kupunguza adha ya upatikanaji wa nishati hiyo na kuvisaidia viwanda vidogo vidogo ambavyo vilikuwa havifanyi kazi sababu ya ukosefu wa umeme wa kutosha kuweza kufanya kazi.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mkoa wa Morogoro kupitia uwekezaji wa kituo hicho utaenda kuwavutia wawekezaji mbalimbali kwenda kuwekeza Mkoani humo kutokana na upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo ya umeme ukiwemo uwekezaji kupitia uchimbaji wa madini aina ya graphite yanayopatikana Wilaya ya Ulanga.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amemuhakikishia Naibu Waziri Mkuu huyo kuwa watatunza vyanzo vya maji maeneo ya hifadhi na kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa wale wote wanaoharibu vyanzo vya maji kwa makusudi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini Mstaafu Meja Jenerali Dkt. Jacob Kingu amesema Bodi ya nishati vijijini kwa kushirikiana na Menejimenti ya wakala wa nishati vijijini itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara na Nishati na kuhakikisha nishati ya umeme nchini inapatikana katika maeneo yote ya vijijini.
Nao wananchi akiwemo Ali Mohamed mkazi wa Kijiji cha Kibaoni kwa niaba ya wananchi wenzake ameishukuru Serikali ya awamu ya sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mradi huo wa kupoza umeme na kwamba utapunguza changamoto ya umeme kukatika mara kwa mara ambapo wataanza kufanya biashara zao za kutumia umeme bila usumbufu.
Ujenzi wa mradi huo ulianza Machi 24, 2020 na kukamilika Machi 31 mwaka huu kwamba mradi huo utazinufaisha Wilaya tatu za Ulanga, Malinyi na Kilombero na kuondoa changamoto ya umeme na kuongeza kasi ya maendeleo ya wananchi wa Wilaya hizo kupitia usindikaji wa mazao ya kilimo, uchimbaji wa madini na kuimarisha huduma za kijamiii.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.