Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameendelea kutekeleza kwa vitendo kampeni ya JISOMESHE NA MKARAFUU kwa kuendelea na zoezi la kugawa miche ya karafuu kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi hao kuweza kutumia mikarafuu kujiendeleza kimasomo.
Katibu Tawala huyo amegawa miche hiyo leo Machi 5, 2025 katika shule za Sekondari za Halmashauri ya manispaa ya Morogoro Mkoani humo akitekeleza kampeni iliyozinduliwa hivi karibuni katika Wilaya ya Morogoro.
Dkt. Mussa amesema zoezi hilo la ugawaji wa miche ni endelevu na linalenga kuwawezesha wanafunzi wa kidato cha kwanza kujisomesha wenyewe kwa kuweza kupata fedha zitakazo wasaidia kununua mahitaji mbalimbali hususan mahitaji ya shule kupitia zao la karafuu baada ya miaka minne ijayo.
".tunachokifanya kama Mkoa kwa sasa hivi ni kuwawezesha nyie wanafunzi kwa manufaa yenu" amesisitiza Dkt. Mussa Ali Mussa.
Aidha, Katibu Tawala huyo amewataka wazazi, Wàlezi na Wanafunzi kupanda miche hiyo maeneo ya nyumba zao na kuisimamia ili iweze kukua na kuweza kuwasaidi wanafunzi katika masomo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bw. Emmanuel Mkongo amesema Halmashauri hiyo imegawa miche 4540 kwa wanafunzi 454 wa Sekondari hususqn wa kidato cha kwanza wa shule 6 za halmashauri hizo.
Naye Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kingalu Bi. Eliza Hamisi kwa niaba ya wanafunzi wenzake ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa kuwapatia miche hiyo huku akiahidi kuitunza ili iweze kumasaidia kumwingizia kipato yeye na wazazi wake na vizazi vijavyo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.