Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Utalii, mamlaka za uhifadhi na kituo cha utangazaji ITV wamewasilisha mpango mkakati wa kuufanya Mkoa huo kuwa wa kiutalii kwa kuainisha vivutio vyote vya utalii vilivyopo katika Halmashauri tisa za Mkoa huo.
Mawasilisho hayo yamefanyika leo Februari 26 mwaka huu katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kikao hicho ni mahususi kwa ajili ya kukuza na kuendeleza utalii na vivutio vingine Mkoani humo.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho amesema lengo kubwa la kikao hicho ni kuweka uelewa wa pamoja wa vivutio vilivyopo katika Mkoa huo, kutambua changamoto na kuweka mikakati ya kuendeleza utalii katika Mkoa na taifa kwa ujumla.
Loata Sanare amesema moja ya lengo la jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za kuendeleza utalii lengo ni kuongeza pato la nchi na kukuza ajira katika Nyanja zote hususan katika usafirishaji, Kilimo, biashara na viwanda na miundombinu mingine.
Aidha, Loata Sanare amebainisha kuwa hadi sasa sekta ya utalii inachangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la taifa na kiasi kidogo ukilinganisha na utajiri wa vivutio na rasilimali vingine vilivyopo katika Mkoa wa Morogoro.
Akitoa taarifa ya hali ya vivutio vya utalii katika Mkoa huo, Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema licha ya fursa nyingi zilizopo katika Mkoa huo, utalii ulikuwa haujapewa kipaumbele hivyo kwa sasa wametambua vivutio vyote vya utalii na kuandaa mwongozo ambao utahusisha mbuga za wanyama na utamaduni yaani vivutio vya asili.
‘’Moja ya fursa ambayo tulikuwa hatujaitumia katika Mkoa wetu ni utalii ambayo kama Mkoa tumejipambanua kwamba tuna maeneo mengi ya utalii, tumeunda kamati kuweza kuandaa andiko la mwanzo la kuangalia ni kwa namna gani tunaweza kuwa na mwongozo wa utalii katika Mkoa wetu wa Morogoro’’ amesema Kalobelo.
Mhandisi Kalobelo amesema kuwepo kwa kikao hicho ni pamoja na kutekeleza maelekezo ya ilani ya uchaguzi ya Chama kilichopo madarakanai - CCM ya mwaka 2020 ambayo imeelekeza katika kipindi hiki kuhimiza masuala ya utalii ili kuongeza pato la taifa.
Sambamba na hayo, Mhandisi Kalobelo ametoa wito kwa wadau wa kikao hicho kufikiria namna Mkoa wa Morogoro unavyoweza kujikuza kitalii kutokana na vyanzo vingi vya kitalii vilivyopo katika Mkoa huo hali itakayopelekea kuinua uchumi wa wananchi wake, Mkoa na Taifa kwa kwa ujumla.
Wakiwasilisha taarifa za vivutio vinavyopatikana katika Mkoa wa morogoro wadau waliohudhuria katika kikao hicho akiwemo Afisa Mhifadhi daraja la pili Mikumi kutoka hifadhi ya taifa ya Mikumi Samwel Mguhachi, amesema hifadhi hiyo ina wanyama watano wakubwa wanaopendwa kuangaliwa akiwemo Simba, nyati, Tembo, Chui na Kiboko.
Akibainisha changamoto zilizopo katika sekta ya utalii Mkoani Morogoro kwa lengo la kutatuliwa ili kuwatengenezea mazingira rafiki watalii kutoka ndani na nje ya Mkoa huo Afisa Wanyamapori wa Mkoa wa Morogoro Joseph Chuwa amesema kuna uwekezaji mdogo katika utalii hususan katika makampuni ya kusafirisha watalii.
Pia, Chuwa amebainisha changamoto nyingine kuwa ni ubovu wa miundombinu, kutotangazwa vivutio vya utalii, uharibifu wa mazingira unaotishia uhai wa vivutio vilivyokuwepo na upungufu wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiutalii.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.