Mwenge wa uhuru 2025 umepokelewa leo Aprili 11, 2025 Mkoani Morogoro kutoka Mkoa wa Pwani na unatarajia kupitia miradi 70 ya maendeleo iliyopo katika halmashauri 9 za mkoa huo yenye thamani ya Tsh. Bil. 18.5.
Hayo yamebainishwa Machi 11, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Alhaji Adam Kighoma Malima wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru uliokamilisha mbio zake katika Mkoa wa Pwani.
Mwenge huo umepokelewa katika kijiji cha Mgude Wilayani Morogoro ukiwa ni Mkoa wa Pili kuupokea tangu ulipozinduliwa na Mhe. Dkt. Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mkoani Pwani Aprili 2 mwaka huu.
Akifafanua zaidi, Mhe. Malima amesema miradi hiyo ya maendeleo inayowagusa wananchi ikiwemo miradi ya afya, mindombinu, elimu, maji na miradi mingine inatarajia kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa wananchi huku akiahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakimbiza Mwenge wa Kitaifa ili waweze kukamilisha majukumu yao ya kukimbiza Mwenge huo.
"...Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Wilaya 7 na Halmashauri 9 za Mkoa wa Morogoro ambapo utazindua pamoja na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo 70 yenye thamani ya Tsh. Bil. 18.5..." Amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa upande wake, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 Bw. Ismail Ali Ussi amewataka watendaji wanaohusika na miradi inayopitiwa na mwenge wa uhuru kuandaa nyaraka za mradi husika na vifaa vingine vya vinavyotumika katika kukagua ubora wa mradi ili kurahisisha ukaguzi wa miradi wakati wa mbio hizo.
Mwenge wa uhuru unatarajiwa kukimbizwa Mikoa 31 hapa nchini, Halmashauri 195 ukiwa na kaulimbiu inayosema "Jitokeze kushiriki uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu".
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.