Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imesema, inakwenda kuishauri Serikali kuiwezesha Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA) kuwa na Maghala makubwa ya kuhifadhia Mbegu na Mitambo ya kisasa ya kuzalishia mbegu ili kuongeza kasi ya kuzalisha Mbegu za mazao ili kuwa tosherevu kwa watanzania.
Hayo yamebainishwa Januari 12, 2025 na Mwenyekiti wa PIC Mhe. Augustine Vuma (MB) wakati wa ziara ya kamati hiyo Mkoani Morogoro ilipotembelea Makao Makuu ya ASA na kujionea hali halisi ya uhitaji wa maghala ya kuhifadhia mbegu zinazozalishwa.
Mhe. Augustine Vuma amesema, kwa sasa ASA wanazalisha 5% tu ya mbegu za mazao zinazopatikana sokoni ukilinganisha na uhitaji wa watanzania hivyo kufanya sehemu ya asilimia kubwa ya uzalishaji huo kutoka nje ya nchi.
”…lakini jambo la pili lazima Serikali ihakikishe kwamba ASA wanapata Mitambo Mizuri na ya kisasa ili aweze kuzalisha mbegu kwa kasi kubwa zaidi,..” amesema Mwenyekiti huyo.
Kuhusu Kiwanda cha mafuta cha MOPROCO cha Mkoani humo ambacho hakifanyi kazi kwa sasa, amesema ni wajibu wao pia kama Kamati kuishauri serikali kuhakikisha inatafuta namna nzuri ya kumaliza sintofahamu iliyopo baina ya aliyekuwa mwekezaji na Serikali kwa kuwa uwekezaji uliofanyika katika kiwanda hicho ni mkubwa hivyo, kuacha majengo yaliyopo sasa bila kutumika ni kuiletea Serikali hasara.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Igunga Mhe. Nicholaus Ngassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya PIC ameipongeza Wizara ya Kilimo chini ya Mhe. Hussein Bashe Waziri wa Kilimo (MB) kwa kusimamia ASA, TARI na TOSCI kufanya kazi kwa ushirikiano hivyo kutimiza ndoto za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kutaka kuwaletea wananchi Maendeleo yao.
Awali, akimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa una dhamira ya kulima mazao Matano ya kimkakati likiwemo zao la Parachichi, Kakao, Mchikichi, Kahawa na mkazo mkubwa upo kwenye zao la Karafuu ambapo hadi sasa Mkoa unazalisha zaidi ya tani 2000 za Karafuu kwa mwaka.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Bw. Nyasebwa Chimagu pamoja na kuishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea Makao Makuu ya ASA, amebainisha malengo ya Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhifadhi tani milioni tatu za mazao ifikapo mwaka 2030 ili muda wote serikali iwe na uhakika wa chakula kwa wananchi wake.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.