Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Taasisi ya The Islamic Foundation kwa kushiriki masuala ya kijamii na kutoa misaada ya sekta ya Afya, Elimu na Maji ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo na kusogeza huduma hizo karibu yao.
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi hizo Novemba 25, Mwaka huu wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Msikiti Masjid Al Gaith uliopo kata ya Kilakala Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo ujenzi ambao hadi kukamilika kwake utagharimu takribani Tsh. Bil. 7.
Mara baada ya kuweka jiwe la msingi Rais Samia amesema Pamoja na kujenga msikiti huo kwa ajili ya ibada ya waumini wake bado anaipongeza taasisi hiyo kwa kutoa misaada mingi kwa watanzania wote kupitia sekta za Afya, Elimu na Maji.
“… niipongeze Taasisi ya The Islamic Foundation kwa mchango wake kupitia miradi kwenye sekta za afya, elimu na maji, kwa kweli hizi ndio sekta mwenyezi Mungu alizotusisitiza kutoa sadaka…” amesema Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiomba taasisi hiyo kuendelea kutoa misaada kwa waathirika wa majanga mbalimbali yanayotokea hapa nchini hususan mafuriko, Matetemeko ya ardhi na njaa ambapo Taasisi hiyo imekuwa kinara wa kutoa misaada kama hiyo.
Sambamba na rai hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan kupitia hafla hiyo amewataka viongozi wote wa dini hapa nchini kuendelea kuhubiri amani, Utulivu na Upendo kwa waumini wao na kuwa kiunganishi ili jamii iweze kuondokana na migogoro isiyokuwa na tija.
Katika hatua nyingine Rais Samia amesisitiza kuwepo kwa ujenzi wa madrasa ili kuwa na waumini wa kutosha wa kutumia misikiti inayojengwa na kuongeza watanzania wenye hofu ya Mungu kwa kupata elimu sahihi ya dini ndani ya kwa jamii kwa kufanya hivyo kutaendelea kuwa na kizazi chenye maadili mema na kutunza amani na utulivu kwa Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya ndani Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika mialiko ya dini zote jambo ambalo amesema linasaidia kulinda na kutunza amani na utulivu kwa watanzania kwani viongozi wa dini wanafanya kazi kubwa ya kuhubiria maadili yaliyo bora.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Kighoma Malima Pamoja na kumshukuru Rais kwa kuendelea kufanya ziara Mkoani humo amebainisha kuwa msikiti huo utakapokamilika Pamoja na kuwa ni nyumba ya ibada bado utakuwa kivutio kikubwa cha utalii ndani ya Mkoa huo.
Naye, Mwenyekiti wa Taasisi ya The Ilsamic Foundation Sheikh Aref Nadhi amesema Mradi huu unamilikiwa na Taasisi ya The Islamic Foundation ambao unafadhiliwa na jumiya ya Dar Al Ber Society iliyopo Dubai Falme za Kiarabu inayojishughulisha kusaidia kutoa huduma za kijamii Tanzania bara na visiwani hususan sekta ya afya, Maji, elimu, Kulea watoto yatima, Ujenzi wa Nyumba za Ibada, kusaidia waathirika wa majanga na kutoa misaada kwa wasiojiweza.
Msikiti huo utakaogharimu takribani shilingi 7 Bil. Hadi kukamilika kwake, utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuchukua waumini 3000 kwa wakati mmoja.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.