Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amelishukuru na kulipongeza jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia shirika la Mzinga kwa kufanikisha zoezi la kutengeneza kifaa saidizi (mguu bandia) chenye thamani ya shilingi milioni 2.5. Kwa ajili ya Mgonjwa aliyemuahidi kumpatia kifaa sqidizi hicho.
Mhe. Adam Kighoma Malima ametoa pongezi hizo Februari 4, 2025 wakati wa tukio la kumkabidhi kifaa saidizi (mguu bandia) Bw. Jackson Mwakalinga tukio lililofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa.
Mhe. Malima amesema, kwa ushirikiano mkubwa na shirika la Mzinga wamefanikiwa kupata kifaa saidizi kwa ndugu Jackson ikiwa ni ahadi ya Mkuu wa Mkoa huyo aliyoitoa Agosti 27, 2024 siku ya Maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ alipotoa ahadi ya kumpatia mgonjwa huyo kifaa saidizi cha kumsaidia kutembea.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ametumia nafasi hiyo kulipongeza JWTZ kwa jitihada zinazofanywa na jeshi la wananchi hasa shirika la Mzinga Mkoani Morogoro kwa kutoa huduma nzuri kwa jamii inayowazunguka zikiwemo huduma za afya.
“…nakushukuru sana Jenerali kwani hiki ni kielelezo cha umahiri na umakini wa jeshi la wananchi wa Tanzania maana jeshi ni jeshi wakati wa vita na ni jeshi hata wakati wa Amani..” Amesema Mhe. Adam Malima
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Shirika la Mzinga na Mkuu wa kikosi MAZAO, Brigedia Generali Seif Athuman Hamisi, akielezea historia ya Hospitali ya kikosi cha Mzinga amesema hospitali hiyo ilianza 1976 kama Zahanati iliyokuwa inatoa huduma kwa maafisa wa Jeshi na hivi sasa ni hospital inayohudumia hata wananchi wa kawaida ngazi ya Wilaya kwa huduma tofauti kama vile utoaji wa huduma za vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu wa viungo.
Naye, Bw. Jackson Mwakalinga ambaye alikatwa mguu wake baada ya kushauriwa na madaktari ili kuokoa uhai wake amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa moyo wake wa kumpambania kupata kifaa hicho cha kumsaidia kutembea huku akilipongeza shirika la Mzinga kwa kufanikisha upatikanaji wa kifaa hicho.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.