Wadau mbalimbali Mkoani Morogoro wametakiwa kuongeza msukumo wa ufaulu kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari ikiwa ni alama ya shukrani na kutimiza ndoto za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za ‘Boost’ mkoani humo.
Hii ni Shule mpya ya Msingi Mgaza iliyojengwa kupitia mradi wa Boost kwa gharama ya shilingi milioni 473.
Hayo yamebainishwa Januari 4, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya Maendeleo ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambapo pia alitembelea shule mbili za BOOST za Halmashauri hiyo kati ya shule 17 zilizojengwa Mkoani humo.
Muonekano wa shule mpya ya msingi ya Viwandani.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Rais Samia ametoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya kupitia mradi wa ‘boost’ ambapo Mkoa huo umefanikiwa kujenga shule mpya 17 na kuwataka wadau Mkoani humo sasa kujielekeza katika kuongeza ufaulu wa wananfuzi kama alama ya shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
“...kwa hiyo tuna shule za Boost 17...tukitaka kumtendea haki Dkt. Samia Suluhu Hassan tuongeze kiwango cha ufaulu cha Watoto”. Amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bw. Ally Machela amesema Halmashauri hiyo imefanya utafiti wa kubaini maeneo ya kujenga vivuko kwa ajili ya kuwarahisishia wanafunzi kufika maeneo wanayosoma wakiwa salama ikiwemo kata ya Mafisa ambapo tayari imeandika barua kuomba kupatiwa mataluma ya kujengea vivuko hivyo.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mh. Pascal Kihanga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan huku akibainisha kuwa kwa kipindi kifupi tangu aingie madarakani ametoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya Afya, Elimu, Maji na Umeme katika Manispaa hiyo.
Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya halmashauri ya manispaa ikiwemo miradi wa Reli ya Kisasa ya umeme ya SGR, Hospitali ya Manispaa na miradi ya maji ya Mamlaka ya Maji na USafi wa Mazingira Mkoa wa Morogoro – MORUWASA.
Kwa upande wa miradi ya Elimu iliyotembelewa na kuwekewa mawe ya msingi ni Pamoja na shule mpya mbili za BOOST za Viwandani na Mgaza, ambapo imebainishwa kuwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa darasa saba mwaka 2023 Mkoani humo ni asilimia 79 ufaulu unaotakiwa kupandishwa zaidi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.