RC MOROGORO AWABANA WAKURUGENZI MADENI YA POSI
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watumishi wa Serikali ambao ni wadaiwa sugu wa fedha za ndani wanazokusanya kwa kutumia mashine za POSI ili kupunguza ama kukomesha kabisa tabia hiyo.
Mhe. Adamu Malima ametoa agizo hilo wakati wa kikao chake na Kamati ya fedha za Halmashauri ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) iliyoagiza Halmashauri zote kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali – CAG.
Akiwa katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima alisikitika kuona kuna baadhi ya halmashauri zina hoja za madeni makubwa ya wadaiwa sugu wa fedha za makusanyo kutoka kwa baadhi ya watumishi wa Serikali huku watumishi hao wakiwa nje bila ya kulipa fedha hizo.
Kwa sababu hiyo, Mkuu wa Mkoa huyo akawaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa huo kutocheka na watumishi wa Serikali wasiowaaminifu wala kuwa na huruma nao, badala yake wawachukulie hatua kali za kisheria kila wanapobainika.
“Wizi wa fedha za POSI wasiachiwe wala kupewa msamaha, wawekeni ndani” alisema Adam Malima.
Sambamba na maelekezo hayo Mkuu huyo wa Mkoa akaiagiza Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa - TAKUKURU Mkoa wa Morogoro kuchunguza wadaiwa hao na kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria lakini pia taarifa zao ziwasilishwe Ofisini kwake.
“…hajawahi kulipa hata senti tano……kafungwa miaka miwili katoka bado hajawahi kulipa hata senti tano, TAKUKURU, nitafutieni Profile ya huyo mtu..” alisisitiza.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa kupitia kikao hicho aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi walio chini yao Pamoja na watumishi wengine.
Kwa upande mwingine akawataka watumishi nao wafanye kazi zao kwa mujibu wa Sheria, taratibu na Kanuni na kwamba mtumishi atakayethibitika kufanya hujuma yoyote kwa Mkurugenzi wake atamchukulia hatua kali za kisheria.
Halmashauri ambazo zimeonekana zina watumishi wa umma ambao ni wadaiwa sugu wa fedha nyingi za Makusanyo ni Pamoja na Halmashauri ya Mlimba, Ifakara, Ulanga, Mvomero na Morogoro DC.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.