Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Rehema Bwasi kupitia Afisa Utumishi wa Halmashauri hiyo Ndg. Kelvin Luvinga kumsimamisha kazi mara moja Mtendaji wa kijiji cha Matuli Bw. Rashid Ponera ili kupisha uchunguzi wa ubadhilifu wa fedha za umma zaidi ya Shilingi Mil.100.
Loata Sanare ametoa agizo hilo Machi 11, mwaka huu wakati wa ziara ya kikazi katika Wilaya ya Morogoro ya kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wananchi ambapo alifika Shule ya Sekondari ya Matuli na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji hicho.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa Rashid Ponela anatuhumiwa kwa kosa la ubadhilifu wa fedha za mradi wa mkaa endelevu uliokuwa unasimamiwa na baadhi ya wanakikundi wa kijiji hicho.
‘’Sasa nikwambie tena, msimamishe leo, Mhe, Mwenyekiti wa chama yuko hapa yule mwenyekiti na yeye mchukulie hatua za kichama nimeshagundua kuna kulindana kwingi hapa’’ amesema Loata Sanare.
Pamoja na kumsimamisha Mtendaji wa Kijiji hicho, Mkuu huyo wa Mkoa pia ameagiza Mwenyekiti wa Kijiji cha Matuli naye achukuliwe hatua za kichama kutokana na tuhuma za ubadhilifu wa fedha za mradi huo wa mkaa endelevu wa Kijiji.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Matuli ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya hiyo Mhe. Lucas Lemomo amesema suala la ubadhilifu wa fedha hizo aliuibua yeye kutokana na wananchi wa kijiji cha Matuli kushindwa kuchangia ujenzi wa Shule ya Msingi Matuli licha ya kuwa na mradi wa mkaa endelevu kijijini hapo.
Sambamba na hayo, Lemomo amebainisha kuwa mbali na zaidi ya Shilingi Mil. 100 zilizofanyiwa ubadhilifu, kuna Shilingi Mil. 23,500,000/= ambazo hazikuingizwa kwenye akauti ya kijiji na hazifahamiki zimetumika vipi na wapi kutokana na vielelezo husika kutowasilishwa kwenye Baraza la Madiwani baada ya kuvihitaji.
Akitoa ufafanuzi wa ubadhilifu wa fedha hiyo Afisa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro Emmanuel Komba amesema wahusika wa ubadhilifu wa fedha hizo wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipa sehemu ya fedha hizo ambapo hadi sasa zaidi ya Shilingi Mil. 2,000,000/= zipo kwenye akauti yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanakikundi wa mradi wa mkaa endelevu uliopo katika kijiji cha Matuli akiwemo Peter John, amempongeza Mkuu wa Mkoa Loata Ole Sanare kwa kumchukulia hatua Mtendaji wa kijiji hicho ili liwe funndisho kwa viongozi wengine.
‘’Binafsi niseme kwamba uamuzi alioufanya kiongozi wetu ni sahihi na naamini utakuwa fundisho kwa viongozi wengine, viongozi wengi wanashindwa kuwa waadilifu hali inayopelekea kutukwamisha kimaendeleo sisi wananchi’’ amesema John.
Mradi wa Mkaa Endelevu katika Kijiji cha Matuli Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ulianza mwaka 2016 na utekelezaji wake ukaanza rasmi mwaka 2017, mradi huo ulikuwa na lengo la kupiga hatua kimaendeleo na kufika mbele zaidi kwa kujitegemea kupitia Mradi huo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.