Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameamuru kukamatwa kwa Daktari Cassius Lwebangira wa Kituo cha Afya cha Mikumi kwa tuhuma ya kumchelewesha mama mja mzito na kusababisha mama huyo kujifungua akiwa ndani ya Bajaji kwa sababu ya kutaka fedha.
Martine Shigela ametoa agizo hilo Julai 27 mwaka huu wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji mdogo wa Mikumi Wilayani Kilosa Mkoani humo ambapo ameendelea kupokea kero za wananchi wa Wilaya hiyo na kuzitatua.
Awali kijana aliyejulikana kwa jina la Abdallah Agustino mkazi wa Mikumi akitoa kero yake Mbele ya Mkuu wa Mkoa alimueleza kuwa mnamo mwezi Aprili mwaka huu alimpeleka mke wake Jenifa Francis katika Kituo cha Afya cha Mikumi akiwa ni mja mzito ili kupata huduma ya kujifungua katika kituo hicho.
Kwa mujibu wa maelezo ya Abdallah Daktari aliyekuwepo zamu Cassius Lwebangira alimueleza Abdallah kuwa mke wake anatakiwa afanyiwe upasuaji na kumtaka ampe fedha kiasi cha shilingi laki moja na ishirini ili atumie vifaa vyake katika upasuaji huo badala ya kwenda kuvinunua sehemu nyngine.
Kwa mujibu wa maelezo ya Abdallah anasema baada ya kushindwa kutoa kiasi hicho cha fedha alimwambia Abdallah achague mawili au kumpe kiasi cha fedha hizo ama kuondoka na mke wake hospitalini hapo huku mama huyo akiwa anahangaika uchungu wa uzazi hali iliyomfanya baada ya muda kujifungua akiwa ndani ya Bajaji njiani wakielekea Kituo Cha Afya cha St. Kizito cha Mikumi.
Akijibu swali la Mkuu wa Mkoa juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya Daktari huyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa George Kasibante alimweleza Mkuu wa Mkoa tayari hatua zilishachukuliwa ikiwa ni pamoja na kubadilisha uongozi wa Kituo hicho cha Afya pamoja na kumpa Onyo mhusika.
Hata hivyo Mhe. Shigela hakuridhika na hatua zilizochukuliwa dhidi ya Daktari huyo ukilinganisha na ukubwa wa kosa alilolifanya na kulazimika kuagiza akamatwe na polisi ili alale rumande huku akimuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro Manyama Tungaraza kufanya uchunguzi juu ya suala hilo kwa kina huku akiagiza akidhibitika na kosa aweze kuchukuliwa hatua nyingine za kinidhamu.
Aidha, Mhe. Shigile ametumia fursa hiyo kuwataka watumishi wengine wa Umma wa Sekta ya Afya Mkoani humo, kuacha mara moja kuwanyanyasa akina mama hasa waja wazito na kwamba jambo hilo halikubaliki kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu Serikali inaleta fedha nyingi kwa ajili ya dawa na vifaa tiba ili kuboresha Afya za wananchi wake.
Mkuu wa Mkoa Martine Shigela yuko kwenye ziara ya kutembelea miradi itakayopitiwa na mwenge wa uhuru 2021. Hadi sasa tayari amefanya ziara hiyo katika Wilaya za Gairo, Kilosa na leo yuko Wilaya ya Morogoro.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.