Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewaahidi ushirikiano Wakufunzi wa sensa ngazi ya Mkoa waliohitimu mafunzo yao leo Julai 26 na kuwataka kwenda kufanya kazi kwa weledi ili kufanikisha zoezi hilo kwa ufanisi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akimkabidhi zawadi ya cheti cha kuhitimu Mafunzo mmoja wa washiriki wa Mafunzo ya Makarani Wakufunzi wakati wa kufunga mafunzo hayo Julai 26 mwaka huu katika Chuo cha WAMO Mkoani Morogoro.
Martine Shigela amesema hayo Julai 26 mwaka huu wakati wa kufunga Mafunzo ya wakufunzi hao ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wakufunzi hao kwenda kuandaa Makarani na Wasimamizi kwa kuzingatia weledi, sheria na kanuni ili kupata Makarani na Wasimamizi makini wa kufanya zoezi hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akihutubia Makarani Wakufunzi wakati wa kufunga Mafunzo hayo.
Aidha, Martine Shigela amebainisha kuwa, zoezi la sensa ya watu na Makazi litafanyika Agosti 22 kuamkia Agosti 23 mwaka huu hivyo kwa wananchi ambao hawatafikiwa na Makarani wa sensa siku hiyo wasipate hofu wowote kwani watafikiwa na Makarani hao ndani ya siku sita kuanzia tarehe tajwa hapo juu ambapo wataulizwa taarifa za wananchi waliolala katika Kaya zao siku ya kuamkia Agosti 23, 2022.
Martine Shigela amebainisha kuwa Kamati ya Sensa ya Mkoa wa Morogoro ina imani kubwa na wakufunzi hao kwani wao pamoja na Makarani na Wasimamizi wa zoezi hilo ndio taswira haswaa ya zoezi la sensa kwa kukusanya takwimu sahihi zitakazosaidia Serikali kuweka mipango yake Katika kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
“Kwa hiyo tuna imani kubwa na Ninyi, mtakwenda kufundisha Makarani watakaofanya kazi yao kwa uadilifu na kujituma, tunaamini mtakwenda kutuletea taarifa zenye ubora unaotakiwa” amebainisha Shigela.
Sambamba na hayo, Martine Shigela amewataka wakufunzi hao kuuwakilisha vema Mkoa wa Morogoro kwa kutembelea maeneo yao ya kazi mapema zaidi ili kurahisisha zoezi hilo wakati wa ukusanyaji wa taarifa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya wa Mkoa huo amesema, Halmashauri za Wilaya Mkoani humo zipo tayari kupokea mafunzo kutoka kwa Wakufunzi hao kwani ndio matumaini yao kwao ya kuwapiga msasa Makarani na Wasimamizi watakaokwenda kwa wananchi wakati wa zoezi la sensa.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuhutubia wahitimu wa mafunzo ya Makarani Wakufunzi.
Kwa upande wake Bw. Athumani Kapate ambaye ni mmoja wa Makarani Wakufunzi ameishauri jamii kuacha tabia ya kuficha watu wenye ulemavu na kusababisha kutokuhesabiwa kitendo kinachopelekea kundi hilo Maalum kukosa haki zao za msingi, hivyo ameishauri kuwapa haki kundi hilo ili kuhesabiwa.
Kamati ya Sensa ya Mkoa wa Morogoro ikiwa katika picha ya pamoja baada ya kufungwa kwa mafunzo hayo.
Baadhi ya Wahitimu wa Mafunzo ya Makarani wakufunzi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Viongozi wengine baada ya kufungwa kwa mafunzo hayo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.