Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema TAMISEMI inatarajia kutoa ajira za watumishi zaidi ya 23000 kwa kada ya elimu na Afya ili kuongeza ufanisi katika Sekta hizo.
Waziri Mchengerwa amebainisha hayo Januari 6 mwaka huu wakati akifunga kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi Elimu na Maafisa Elimu wa Halmashauri hapa nchini kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Glonency iliyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Waziri huyo amesema, TAMISEMI imepokea kibari cha ajira mpya kwa kada ya elimu na Afya lengo ni kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu na wahudumu wa afya hapa nchini na kwamba ajira hizo zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
"...kwa mwezi huu wa Januari na Februari Ofisi ya Rais TAMISEMI tunachokibali cha ajira na tutatangaza hivi punde ajira za walimu na maafisa afya karibu 23000... " amesema Waziri Mchengerwa.
Aidha, Waziri Mchengerwa amebainisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu hadi sasa kwa Serikali hii, kupitia mradi wa kuboresha miundombinu ya elimu ya Awali na Msingi yaani "Boost" Serikali imepanga kutumia trilioni 1.15 kwa ajili ujenzi wa madarasa 12000 na matundu ya vyoo 6000 ifikapo 2025, hadi sasa Serikali imejenga shule mpya za msingi 302 na madarasa 1668 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 230.
Aidha, imepanga kutumia shilingi 1.2 bilioni kupitia mradi wa uboreshaji miundombinu ya elimu ya sekondari "SEQUIP" ambapo itajenga shule mpya za sekondari za kata 1000 na hadi sasa imejenga shule mpya za sekondari 26 za wasichana na shule mpya 443 za sekondari za Kata na zinatarajia kupokea wanafunzi mwezi Januari mwaka huu.
Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa amewataka Wazazi na Walezi kuwaandikisha watoto wao walio katika umri wa kuanza darasa la awali na darasa la kwanza ili waweze kupata elimu kwani Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeondoa kikwazo cha ada.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa umejielekeza katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa Mkoa huo kutoka asilimia 79 ya ufaulu wa mwaka 2023 kufikia asilimia 90 na zaidi.
Aidha, amebainisha kuwa sekta ya elimu Mkoani humo imepata zaidi ya shilingi bilioni 37 ambazo zinatekeleza miradi mbalimbali ya elimu ambapo shule mpya 18 na madarasa 164 ujenzi wake umekamilika na kuongeza kuwa katika muhula mpya wa masomo unaotarajia kuanza Januari 8, 2024 Mkoa unatarajia kusajili jumla ya wanafunzi 84600 wa darasa la awali na darasa la kwanza.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Tamisemi - Elimu Dkt. Charles Msonde amewapongeza Maafisa Elimu hapa nchini kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha elimu hapa nchini ambayo itasaidia kukuza sekta ya elimu ikiwemo kuwapandisha madaraja na vyeo walimu, kuimarisha umahiri wa K tatu yaani Kusoma, Kuandika na kuhesabu na kutekeleza kwa vitendo Sera na Mitaala mipya ya elimu ambayo inatarajiwa kuanza kufundishwa Januari 8 mwaka huu.
Kikao kazi hicho cha siku tatu kilijumuisha Makatibu Tawala Wasaidizi Sehemu ya Elimu na Maafisa Elimu wa Halmashauri zote hapa nchini, ambapo kililenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu yao kupitia vigezo na malengo waliyojiwekea.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.