Wananchi wilayani kilosa na manispaa ya morogoro mkoani humo, wametakiwa kutunza miundombinu ya barabara inayojengwa na Serikali ikiwa ni pamoja na vyuma vya madaraja ili miundombinu hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu kwa faida yao na vizazi vijavyo.
Wito huo umetolewa Machi 10, 2024 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa wakati wa ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo ya kutembelea Miradi ya maendeleo ya sekta ya miundombinu hususan barabara zinazojengwa katika Wilaya hizo.
Dkt. Mussa Ali Mussa ambaye amemwakilisha mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima amesema, serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo lakini kuna watu wachache ambao wanarudisha nyuma azma ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo na kuwataka kwa umoja wao kuwa walinzi wa miundombinu hiyo.
Akiwa katika daraja la Berega Wilayani Kilosa Dkt. Mussa amewataka wananchi wanaoishi Berega na vijiji jirani na daraja hilo ambalo linaunganisha mikoa miwili ya Morogoro na Tanga kuungana na kupanda miti pembezoni mwa mto wa daraja hilo kwa ajili ya kuimarisha daraja hilo ikiwa ni pamoja na kupanda mikarafuu ambayo pia ni faida kwao.
Katika ziara hiyo, Wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Katibu Tawala huyo walitembelea miradi ya barabara ya Mfungua kinywa na Kichangani Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, daraja la mto Berega, Daraja la Mazinyungu Ilonga barabara ya Rudewa - Kilosa na daraja la Ruaha Mkuu na daraja la Ruhembe barabara ya Mikumi - Ifakara Wilayani Kilosa.
Wajumbe hao wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wanaendelea na ziara yao katika Wilaya ya Kilombero kwa lengo la kutembelea barabara ya Kibaoni Ifakara, ujenzi wa daraja la Chiwachiwa na ujenzi wa barabara ya Ifakara Mbingu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.