Wtumishi wa mahakama kote nchini wametakiwa kufanya maandalizi ya mapema kabla ya kustaafu ili kutengeneza mazingira mazuri yatakayowasaidia baada ya kupewa fedha zao.
Kauli hiyo imetolewa Julai 26 mwaka huu na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Edward Nkembo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watumishi wa mahakama ya Tanzaniya yanayofanyika kwa siku tano katika ukumbi wa Magadu uliopo katika halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Nkenda amesema ni vyema mtumishi kuweka mipango mkakati ya kufanya maandaliza ya kustaafu tangu anapoajiriwa ikiwa ni pamoja na kuainisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo haitawapelekea kuwa tegemezi.
Aidha, Nkenda amebainisha kuwa wastaafu wengi wamekuwa wakiishi muda mfupi baada ya kustaafu kutokana na matumizi mabaya ya fedha zao ambapo mara nyingi fedha hizo huzitumia kinyume na utaratibu ambao wanakuwa wamejiwekea kabla ya kustaafu.
‘’Changamoto kubwa zinazowakabili watumishi baada ya kustaafu ni kushindwa kupata mahitaji ya lazima, kutapeliwa mafao yao, kupokea maoni mbalimbali ya kufanya biashara ambazo zinamaliza pesa zao na kubadili tabia zao kisha kuishi maisha ya starehe’’ amesema Nkenda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mafunzo hayo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Ndg. Nuhu Mtekele amesema pamoja na mafunzo watakayopatiwa katika semina hiyo, washiriki hao watapata fursa ya kutembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo – SUA kilichopo Mkoani humo ili kujionea kwa vitendo miradi na shughuli za ujasiliamali na uwekezaji katika kilimo, uvuvi na ufugaji.
Ndg. Mtekele amesema kufanya ziara katika Chuo hicho kutawajengea uwezo watumishi hao kutambua aina ya kazi ambayo wanaweza kuifanya mara baada ya kustaafu ili kuwaletea maendeleo binafsi pamoja na jamii iliyowazunguka kwa jumba.
Kwa upande wake Nestory Mujunangoma, ambaye ni Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Morogoro ametoa rai kwa watumishi hao kutojihusisha katika miradi mikubwa ambayo watashindwa kuiendesha na badala yake wajikite katika miradi midogo ikiwa ni pamoja na ujasiliamali ambao utawaletea faida kubwa ya kujikwamua na umaskini.
Sambamba na hayo, amewashauri watumishi hao kujali Afya zao, kuepuka madeni yasiyo ya lazima, kutoendekeza anasa na kuishi vizuri katika jamii ili thamani ya kustaafu iweze kuonekana mbele ya familia zao na Jamii kwa jumla.
Mafunzo hayo ya siku tano ya kustaafu ni sehemu ya utekelezaji wa sera wa mafunzo ya utumishi wa umma ya mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya Mwaka 2019 pamoja Mpango Mkakati wa Chuo wa Miaka mitano wa Mwaka 2018/2019 hadi 2020/2023.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.