Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Wauguzi wote hapa nchini kutoa huduma nzuri kwa wagonjwa, ukarimu na kuwa na majitoleo ili kundoa lawama za wananchi zinazoelekezwa kwa Serikali.
Mhe. Mchengerwa ametoa agizo hilo Januari 8 mwaka huu wakati akikabidhi magari 6 kwa Mganga wa Mkoa wa Moroboro na Halmashauri za Mkoa huo makabidhiano yaliyofanyika hoteli ya Glonency iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Mchengerwa amesema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kuboresha maslahi ya wauguzi hapa nchini hivyo amewataka kuwahudumia wagonjwa kwa ukarimu, bidii na kutanguliza majitoleo katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa hususan wajawazito kama alama ya shukrani kwa Rais Samia.
"...niwaombe sana mkaishi katika maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan...tunategemea ninyi mkafanye kazi nzuri katika maeneo yenu...wahudumieni watanzania, wakija wakina mama wajawazito wahudumieni kwanza maswali baadaye .." amesema Waziri Mchengerwa.
Aidha, amewataka Waganga wa Mkoa na wa Halmashauri hapa nchini kuyatumia magari waliyopewa kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali ya kufuatilia na kusimamia huduma za Afya katika maeneo yao pamoja na kusikiliza kero za wauguzi wao na kuzitatua.
Akibainisha ununuzi wa magari hayo Mhe. Mchengerwa amesema magari hayo yamegharimu shilingi bilioni 52.38 kwa ajili ya Waganga wakuu wa Mikoa na waganga wakuu wa Wilaya huku akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hadi sasa imenunua kwa mpigo magari 528 ya kuhudumia wagonjwa huku kukiwa na mpango wa kununua magari ya kubebea wagonjwa "ambulance" kwa kila jimbo la uchaguzi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutowaacha nyuma wananchi wa Mkoa huo hususan katika Sekta za Maji, Afya na Elimu na kumuomba Waziri Mchengerwa kufikisha shukrani za wanamorogoro kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan huku akiahidi kuwa Mkoa unaenda kuongeza kasi ya ufanisi kupitia rasilimali anazozitoa kwa wananchi wa Mkoa huo.
Magari yanayotolewa sasa ambapo kwa Mkoa wa Morogoro umepata magari 6 ni mgao wa awamu ya kwanza ambapo Waganga wa Halmashauri za Morogoro, Kilosa, Malinyi na Ulanga zimepata magari hayo pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.