Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB), amezitaka Mamlaka za Serikali za Mikoa na Wilaya kuhakikisha zinabainisha vyanzo vya maji, kushirikisha wananchi wanaoishi karibu na vyanzo hivyo, na kuvipa ulinzi kwa kutunga sheria ndogo za kulinda vyanzo hivyo ili kuondokana na uharibifu wa vyanzo hivyo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Machi 5, 2025, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Bwawa la Kidunda, lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mkoani humo ujenzi unalenga kuboresha upatikanaji wa maji katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tanga.
Mhe. Majaliwa amesema ipo haja ya mamlaka hizo kutambua vyanzo vya maji katika maeneo yao ili kuweka mikakati ya kuvilinda na kuzuia uharibifu wa vyanzo hivyo kwa maslahi mapana ya Taifa na kusisitiza Mamlaka za Maji kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na kuwataka wakulima na wafugaji kuendelea kufanya shughuli zao pasipo kuathiri vyanzo hivyo.
"Nazitaka Mamlaka za Mikoa na Wilaya zifanye kazi ya kubainisha vyanzo vyote muhimu vinavyotiririsha maji na kutuletea maji kwenye maeneo yetu," amesisitiza Mhe. Kassim Majaliwa.
Sanjari na hayo, Waziri Mkuu amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi ws bwawa la kidunda kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na kwa viwango vya ubora vinavyotakiwa huku akiwataka wananchi wanaozunguka mradi huo kuwa walinzi namba moja wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa bwawa hilo ili kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Majaliwa amewataka wananchi wa mkoa wa Morogoro kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kuishi huku wakiheshimiana kwa kuwa wote wanategemeana na kukemea tabia ya baadhi ya wafugaji kulisha mifugo yao mashamba ya wakulima na kwamba jambo hilo kamwe halikubaliki.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amesema lengo la Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama, Hivyo ameitaka Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kutosubiri kukamilika kwa ujenzi wa bwawa hilo la Kidunda na kutoa wiki moja timu ya mamlaka hiyo iende Tarafa ya Ngerengere kuhakikisha wanatafuta maji kwa ajili ya wananchi wa Tarafs hiyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, akitoa Salam za Mkoa amesema, hadi Februari 2025, wastani wa upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Morogoro ni takribani 70% huku akibainisha kuwa Mkoa huo una miradi ya maji ya RUWASA yenye thamani ya shilingi bilioni 90, miradi ya maji ya MORUWASA ina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 20, na miradi mingine ina thamani ya shilingi bilioni 75 na kwamba hiyo yote ni jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kumtua mwanamke ndoo kichwsni.
Ujenzi wa Bwawa la Kidunda ambao kwa sasa umefikia 28% hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 335, na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na unatarajiwa kukamilika Disemba 2026. Mradi huo unatekelezwa na Serikali Kuu kupitia Wizara ya Maji na kusimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.