Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara kuandaa mafunzo yanayohusu sheria za Manunuzi kwa ajili ya madiwani wa Halmashauri hiyo ili kuwa na uelewa wa kutosha kwa lengo la kusimamia vema fedha za Halmashauri yao.
Mhe. Adam Malima ametoa hilo Juni 9, 2025 wakati wa kikao cha Baraza Maalum la Madiwani cha kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesaba za Serikali (CAG) kilichofanyika katika Mji mdogo wa Ifakara ambapo hoja 18 zilizotakiwa kujibiwa hoja 12 zinazohusu masuala ya manunuzi.
“Hoja za manunuzi lazima madiwani wawe wanapigwa semina mara kwa mara ili kufungua macho yao kwenye masuala ya msingi…” Amesisitiza Mhe. Adam Malima.
Amesema, mafunzo hayo yatasaidia madiwani kusimamia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na maeneo mengine na kujua jinsi ya kuwasimamia wataalam hususan katika kipindi hiki cha matumizi ya mifumo ili kugundua na kuchukua hatua haraka pale upotoshwaji unapotaka kutokea.
Naye Mkaguzi wa nje wa Mkoa wa Morogoro Bw. Baraka Mfugale amesema hoja za manunuzi zilizokosewa katika taratibu za manunuzi zitafutwa baada ya kufanyika ukaguzi na kubaini tatizo hilo halipo tena.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa amesema maagizo yote yaliyojitokeza kwenye kikao hicho cha Baraza atayasimami na atakaa na watendaji wake katika kuhakikisha hoja za CAG zinapatiwa ufumbuzi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mhe. Kassim Nakapala amesema licha ya mapungufu ya uwepo wa hoja nyingi za CAG katika Halmashauri hiyo bado halmashauri ya Ifakara haijawahi kupata hati chafu jambo ambalo linaakisi utendaji kazi mzuri wa Baraza la Madiwani.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Sainari, Mhe. William Walioto, ameunga mkono wito uliototlewa na Mkuu wa Mkoa wa kuwa na mafunzo ili kuwapa nguvu madiwani katika kusimamia fedha za maendeleo. Pia alibainisha kwamba ugeni wa mifumo kwa maafisa manunuzi umechangia kuchelewesha utekelezaji wa miradi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.