Kamati ya Kudumu ya bunge viwanda, biashara, kilimo na mifugo chini ya mwenyekiti wake Mhe. Deo Mwanyika (MB) imeiagiza Wakala wa Uzalishaji na Usambazaji wa mbegu nchini (ASA) kusafisha mashamba ya kuzalisha mbegu ambayo kwa sasa ni mapori ili yaweze kutumika na kusaidia kuongeza kasi ya uzalishaji wa mbegu na kukidhi mahitaji ya wakulima.
Agizo hilo limetolewa Februari 18, 2025 na Mhe. Mwanyika ambaye ni mwenyekiti wa Ka ati hiyo ya kudumu wakati wa ziara ya kutembelea Kituo cha ASA kilichopo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
Mhe. Mwanyika amesema, kutokana na kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa mbegu hapa nchini ameitaka ASA kufufua mashamba ambayo yalikuwa yanatumika katika uzalishaji wa mbegu ambayo yatasaidia katika uzalishaji wa mbegu na kupunguza uhitaji wa serikali kuagiza mbegu kutoka nje ya nchi.
"..Hatutaki kuona mashamba ya mbegu ambayo ni mapori" Amesisitiza Mhe. Deo Mwanyika.
Aidha kiongozi huyo ameitaka ASA kuhakikisha wanatunza miundombinu ya uzalishaji yakiwemo matrekta na vifaa vingine ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kuleta faida kwa taifa la leo na hata la kizazi kijacho.
Kwa upande wake Naibu waziri wa kilimo Mhe. David Silinde amesema Serikali inafanya jitihada ya kuhakikisha uzalishaji wa mbegu unaongezeka ili kupunguza changamoto ya uhaba wa mbegu kwa wananchi ambapo kwa sasa mbegu zinaagizwa kutoka nje ya nchi hivyo amezitaka taasisi za uzalishaji mbegu na usambazaji kuongeza uzalishaji wa mbegu hizo hapa nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amekitaka kituo cha utafiti wa Mbegu Tanzania (TARI) kuendelea kufanya Tafiti mbalimbali za uzalishaji wa mbegu ili kuweza kuongeza uzalishaji wa mbegu katika maeneo mengi na kukidhi uhitaji wa mbegu kwa watanzania wote.
Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge viwanda, biashara, kilimo na mifugo itendelea na ziara yake Februari 19,2025 katika Halmashauri ya Mji ifakara.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.