Wahariri wa vyombo vya habari hapa nchini wamepewa mafunzo ya usimamizi wa mnyororo wa ugavi ili kuhakikisha wanatambua athari zinazoweza kujitokeza kutokana na ukosefu wa usimamizi madhubuti wa shughuli zote katika mnyororo huo, kwa kuwa huo ndio msingi kwa maendeleo ya nchi.
Hayo yamebainishwa juni 17, 2025, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo wakati akifungua mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika mkoani Morogoro ambapo amesisitiza umuhimu wa mafunzo hayo kwa wahariri kuielimisha jamii kuhusu usimamizi bora wa mnyororo wa ugavi.
Bi. Omolo amesema kuwa kutambua athari zinazotokana na kutosimamia ipasavyo mnyororo wa ugavi kutawawezesha wahariri kutoa miongozo na mikakati madhubuti ya utekelezaji ili kuimarisha usimamizi na kuepuka hasara zinazoweza kujitokeza.
“Nawasihi kutumia jukwaa hili kama fursa muhimu ya kujifunza, kujadili na kubadilishana uzoefu, pamoja na kutoa ushauri kuhusu masuala ya usimamizi wa shughuli za mnyororo wa ugavi,” amesema Bi. Jenifa Christian Omolo.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kutokana na kukosekana kwa miongozo thabiti ya uendeshaji wa shughuli za mnyororo wa ugavi kama vile ununuzi, ugomboaji, uondoaji, upokeaji, urejeshaji, utunzaji, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa.
Aidha Bi. Omolo amesisitiza kuwa ushirikishwaji kwa vyombo vya habari katika masuala hayo utasaidia kuielimisha jamii na kuwezesha serikali kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti hasara zinazojitokeza.
Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi kutoka Wizara ya Fedha Fedrick Mwakibinga amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea wahariri uelewa wa kina na uwezo wa kufikisha taarifa sahihi na kwa wakati ili kuleta uelewa mpana kwa Watanzania kuhusu mnyororo wa ugavi.
Ameongeza kuwa fedha zinazotumika kununua bidhaa na huduma za serikali zinatokana na kodi za wananchi, hivyo ni lazima kuhakikisha matumizi ya fedha hizo yanakuwa ya ufanisi kwa kuimarisha shughuli zote za mnyororo wa ugavi.
Naye Mhariri kutoka Kituo cha Redio Five cha Arusha, Bi. Ashura Mohamed, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha kazi zao za uandishi na uhariri wa habari, ili kuhakikisha Watanzania wanapata habari bora. Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanawajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.