Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, kilimo na Mifugo Mhe. Deo Mwanyika (MB) ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Morogoro chini ya Mkuu wa Mkoa huo Adam Kighoma Malima kwa kuja na ubunifu wa kampeni ya "Jisomeshe na Mkarafuu" ambayo itaenda kuinua kipato cha wanafunzi na kuweza kupata mahitaji yao ya msingi ikiwemo Elimu.
Mhe. Mwanyika ametoa pongezi hizo wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ya JISOMESHE NA MKARAFUU iliyozinduliwa katika Kata ya Mkuyuni Mkoani humo kwa kuwapatia wanafunzi 800 wa kidato cha kwanza miche 10 kila mmoja ili iweze kuwasaidia wanafunzi hao katika maisha yao ya baadae hususan katika safari yao ya Elimu kwa kulima zao hilo la karafuu.
Mhe. Mwanyika amesema, Serikali ya Mkoa wa Morogoro kupitia Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima imechukua maono ya Mhe. Rais na Wizara ya kuhakikisha na kutekeleza agenda ya kilimo ifikapo 2030, pia kuhakikisha bei elekezi ya mazao ya viungo yanasimamiwa ipasavyo ili kuwainua wananchi kiuchumi.
"Nakupongeza sana Mhe. Mkuu wa Mkoa huu ni ubunifu mkubwa na mimi niseme tu ukweli hapo nitaiga" amesema Mhe. Deo Mwanyika.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kuna umuhimu wa kuongeza elimu ya ugani kwa wazazi ili kuondokana na changamoto ya kufa kwa baadhi ya miche ya karafuu huku akitoa ahadi kwa Mhe. Rais kuwa ndani ya miaka mitano Mkoa wa Morogoro utakuwa eneo la uzalishaji namba mbili wa karafuu duniani.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. Mussa Ali Mussa akielezea umuhimu wa kampeni hiyo amesema kampeni hiyo inalenga wanafunzi wa kidato cha kwanza kupanda miche hiyo ili kuwasaidia wanafunzi hao kujisomesha wenyewe kupitia zao la karafuu kwa kuuza karafuu hivyo pia kukuza uchumi wa familia zao, Mkoa na Taifa kwa ujumla na ututunzaji wa mazingira.
Naye Pascal Petro Gabriel mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya Sekondari ya Mkuyuni amesema wameipokea kwa moyo mmoja kampeni hiyo na kwamba miche hiyo itawasaidia kipindi cha masomo na hata baada ya masomo.
Baada ya uzinduzi wa Kampeni ya JISOMESHE NA MKARAFUU katika kata ya Mkuyuni Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Kamati ya Bunge ya Viwanda Biashara kilimo na Mifugo imeendelea na ziara yake ya kukagua shughuli za kilimo katika Kata ya Tawa, ziara hiyo inaendelea Februari 18, 2025 katika Wilaya ya Kilosa na Kilombero.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.