Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro zilizo karibu na hifadhi za Taifa kutenga maeneo maalum isiyo na migogoro na yenye usalama kwa ajili ya uwekezaji.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Februari 20, Mwaka huu, katika Mkutano wa Wawekezaji wa Mkoa wa Morogoro uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Cate Hotel iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akifafanua zaidi, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa wawekezaji wakubwa huvutiwa na miundombinu bora kama vile barabara, viwanja vya ndege na usalama wa maeneo husika, hali inayoweza kuchochea kirahisi ujenzi wa hoteli za kisasa kwa ajili ya watalii.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amewataka wawekezaji wa Mkoa wa Morogoro kuwa wabunifu na kuzalisha bidhaa, huduma na mazao yenye ubora wa juu kwani Mkoa huo una rasilimali nyingi zinazotosheleza mahitaji makubwa ya uwekezaji.
Hivyo kuongeza kuwa wawekezaji kuwekeza katika maeneo yanayozunguka hifadhi kutokana na ongezeko la watalii katika Mkoa huo baada ya watalii wengi kuongezeka kwa sababu ya uwepo wa Reli ya SGR, viwanja vya ndege na barabara, kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Binilith Mahenge, amesema Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa Mikoa bora kumi kuwa na idadi ya miradi ya uwekezaji ambapo Mkoa huo ni wa saba na una miradi 22 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Marekani 447.5.
Mwaka 2024, Kituo hicho cha uwekezaji cha TIC kilikadiria Mkoa huo kuwa na idadi ya miradi 45 ya uwekezaji lakini hadi sasa Mkoa huo una miradi 22 ya uwekezaji iliyosajiliwa, ikiwemo miradi ya kilimo, viwanda, utalii na usafirishaji.
Naye, Meneja wa TIC Kanda ya Mashariki, Bi. Grace Lemunge, amesema kuwa kikao hicho kinalenga kuwaelimisha wawekezaji kwa kuwapatia taarifa kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana katika Halmashauri za Mkoa wa Morogoro.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.