Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima, amewataka wadau wa maji Mkoani humo na wanamorogoro kwa ujumla, kushirikiana katika kutunza vyanzo vya maji vinavyopatikana Mkoani humo kwa ajili ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.
Mhe. Adam Malima amebainisha hayo wakati wa kikao cha wadau wa maji Mkoani humo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Morena iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema, miaka 50 iliyopita, idadi ya watu ilikuwa milioni 15 na rasilimali za maji zilitosha mahitaji ya wananchi, kwa sasa idadi ya watu imeongezeka hadi milioni 65, hivyo kumeongeza mahitaji ya maji kwa matumizi ya shughuli za kibinadamu na kutaka ushirikiano katika kutunza vyanzo vya maji.
"...Miaka 50 iliyopita nchi nzima kulikuwa na watu milioni 15 ambapo maji yalitosheleza sasa wapo watu zaidi ya milioni 65, hivyo kumekuwa na uhitaji wa maji, tunapaswa kushirikiana, kulinda na kutunza vyanzo vyetu kuepuka vita ya maji siku zijazo..."
Pamoja na ukweli kuwa Mkoa wa Morogoro ni moja ya mikoa yenye utajiri mkubwa wa vyanzo vya maji, huku Bwawa la Kidunda likitajwa kuwa litakuwa mhimili mkuu wa nishati ya umeme hapa nchini, bado amewataka wanasiasa kutoingilia masuala msingi ya rasilimali maji, ili kuhakikisha uhifadhi wa vyanzo vya maji unalindwa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amewaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashuri zote za Mkoa huo kulipa kipaumbele suala la kulinda vyanzo vya maji na kulifanya kuwa ajenda namba moja katika vikao vyote vya kisheria wanavyovifanya katika maeneo yao.
Sambamba na hayo, Mhe. Adam amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwani wananchi zaidi ya milioni 3.6 wa Morogoro wanategemea upatikanaji wa maji bora kwa matumizi yao ya kila siku.
Awali, Mkurugenzi msaidizi wa sera, tafiti na ubunifu wa Wizara ya Maji Bw. Alex Tarimo akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu kutoka Wizara hiyo amesema mwaka 1960 upatikanaji wa maji kwa kila mtu ulikuwa wa meta za ujazo 12600 hadi kufikia 2025 hali ya upatikanaji wa maji umekuwa meta za ujazo 1980, hivyo amewasisitiza wadau wa maji na mazingira kushirikiana kulinda na kuendeleza vyanzo hivyo vya maji.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Sospeter Lutonja amesema kikao hicho kimeitishwa mahsusi kwa ajili ya kutathmini miradi iliyotekelezwa ili utekelezaji huo uweze kufikia 85% kama ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyoelekeza.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami - Ruvu Elibariki Mmasy amesema, katika Mkoa wa Morogoro, bodi hiyo imefanya utafiti maeneo ya Manispaa ya Morogoro na kubaini uwepo wa akiba ya maji lita 34,000, huku eneo la Dakawa likiwa na kiasi cha kati ya lita 10,000 hadi 93,000.
Katika bajeti ya mwaka 2024/2025 serikali imetoa Tsh. Bil. 16 kwa ajili ya miradi ya maji lengo ni kumtua Mama ndoo kichwani.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.