Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifubo, Mhe. Deo Mwanyika (MB) amewahakikishia wawekezaji wa ndani kuvilinda viwanda vyao na kuagiza Uongozi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero kuanza uzalishaji wake wa sukari bila hofu yoyote.
Mwenyekiti huyo amebainisha hayo Februari 19 mwaka huu akiwa katika kiwanda cha sukari cha Kilombero Mkoani Morogoro yeye na wajumbe wa Kamati hiyo wakiendelea na ziara yao ya siku sita Mkoani humo ikiwa leo ni siku yao ya tano ya ziara hiyo.
Mhe. Mwanyika amesema kuna umuhimu mkubwa wa Serikali kuwalinda wawekezaji wa ndani pia kulinda viwanda vya ndani ili kuleta chachu ya uzalishaji wa bidhaa ili nchi iweze kusafirisha bidhaaa hizo katika nchi mbalimbali.
"..Lazima tuhakikishe kwamba wawekezaji wetu tunaendelea kuwalinda " Amesema Mhe. Deo Mwanyika.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (MB) amesema Serikali imejizatiti kuwalinda wawekezaji wazawa kwa kuwekeza na kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa hapa nchini kwani amesema hiyo ndiyo sera ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake na kwamba kwa kufanya hivyo tutaondokana na umaskini na kwenda katika hatua nyingine ya kiuchumi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kwa Mkoa wa Morogoro uzalishaji wa Mpunga ni chini ya Tani 1000,000 hivyo Serikali inaendelea kuboresha maiundombinu kwa kuwavutia wawekezaji wa zao la mpunga kuwekeza ili kuongeza tija ya zao hilo na kuongeza uzalishaji wa zao hilo la mpunga,
Pia Mhe. Malima amemshukuru mwekezaji wa kiwanda kidogo cha kuchakata mpunga kwa kuweza kutoa ajira kwa watoto waliozaa mapema ambapo ni moja ya maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rias wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha wanawake hao wanawezeshwa kiuchumi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.