Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele ametoa rai ya kuwataka wananchi wa Mkoa wa Morogoro kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la mpiga kura ifikapo Machi Mosi, 2025 kwani amesema hiyo ndio njia pekee ya kushiriki uchaguzi mkuu ujao wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Mwenyekiti Mwambegele ametoa rai hiyo Februari 18, mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya siku 2 kwa watendaji ngazi ya Wilaya kuhusu uboreshaji wa daftari la mpiga kura yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Magadu iliyopo Manispaa ya Morogoro yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo watendaji hao kwa kutumia mfumo wa kisasa ujulikanao kama Votes Regislation System (VRS).
Aidha, Jaji Mwambegele amewataka watendaji hao kushirikiana na wataalam wengine wa Serikali waliopo katika maeneo yao pamoja na wananchi katika kutoa Elimu ya kutumia mfumo huo wa kisasa ili kufanikisha kwa ufanisi zoezi la uboreshaji taarifa zao ili kushiriki uchaguzi huo mkuu.
Sambamba na hayo, Jaji Rufaa Jacobs amesema kuwa wakati wa uboreshaji wa daftari hilo la kudumu, mawakala wa vyama vya siasa watapata nafasi ya kuwepo kwenye vituo vya uandikishaji huku akiwataka kutoingilia kazi za watendaji wa vituo vya kujiandikishia wapiga kura kwenye vituo watakavyopangiwa.
”….wakati wa uboreshaji wa daftari, mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo kwenye vituo vya kujiandikishia wapiga kura jambo hili ni muhimu kwani litasaidia kuleta uwazi katika zoezi nzima" amesema Jaji Mwambegele.
...lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutotokea vurugu zisizo za lazima". Ameongeza.
Sambamba na ushauri huo Jaji Mwambegele amesema tume imetoa vibali kwa asasi za kiraia 157 kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura pia imetoa kibali kwa taasisi na asasi za kiraia 42 kuwa waangalizi watakao shiriki katika zoezi zima la uandikishaji, taasisi 9 kati ya hizo ni za kimataifa na 33 ni kutoka ndani ya nchi.
Kwa upande wake, Afisa muandikishaji wa Jimbo la Morogoro Mjini Bw. Faraja Madugu, amesema zoezi hilo ni la muhimu kwani ndio kitovu cha ufanisi wa zoezi zima ambapo wapiga kura watapata fursa ya kuchagua viongozi wanaoona wanawafaa katika kuwaletea maendeleo.
Zoezi la uandikishaji ambalo kitaifa lilifunguliwa Mkoani Kigoma linakwenda na kaulimbiu isemayo “kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora”
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.