Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesema uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utaanza kufanyika rasmi Machi 01 had 07, Mwaka huu Mkoani Morogoro. ili kupata fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Novemba, 2025.
Jaji Mwambegele amethibitisha hayo Februari 17, Mwaka huu katika Mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa hoteli ya magadu iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Aidha, Mwenyekiti huyo amesema Tume hiyo imeanza maandalizi wa uboreshaji wa daftari la mpiga kura ambapo itahusisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki (BVR) ili kurahisisha uboreshaji huo na kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya wapiga kura.
“Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa Tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 12 kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa Daftari. Mzunguko huu wa 12 unahusisha Mkoa huu wa Morogoro” amesema Jaji Mwambegele.
Vilevile, Jaji huyo amesema Tume hiyo imekamilisha zoezi hilo katika Mikoa 27 ikiwemo Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida. Mikoa mingine ni Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Kwa sababu hiyo, Jaji Jacobs amewasisitiza wadau mbalimbali kuhamasisha wananchi na kutoa elimu ili kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kurekebisha na kuboresha taarifa zao huku akiwataka wazee, watu wenye walemavu, wagonjwa, wajawazito na wakina mama wenye watoto wachanga watapewa kipaumbele.
Kwa upnde wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Bw. Kailima Ramadhani amesema Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 302,752 Mkoani Morogoro sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 1,612,952 waliokuwepo kwenye daftari la wapiga kura mwaka 2020.
Naye, Balozi Omar Mapuri ambaye ni Mjumbe wa Tume hiyo amesema Tume itazingatia usimamizi wa katiba, sheria na kanuni za uchaguzi katika zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa Taifa la Tanzania huku akiwataka wadau wa uchaguzi kushirikiana na wananchi kwa kuwapa elimu ya uboreshaji taarifa zao.
Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura ambapo uzinduzi wake ulifanyika Mkoani Kigoma Julai 20, Mwaka huu lenye kaulimbiu isemayo "Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora".
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.