Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wananchi wa Mkoa huo kushiriki kikamilifu katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani ambapo kwa Mkoa wa Morogoro kilele cha maadhimisho hayo ni Machi 8, 2025 katika Wilaya ya Kilombero yakiambatana na kaulimbiu isemayo "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji."
RC Adam Malima ametoa wito huo leo Februari 14, 2025 wakati wa Mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo huku akiwataka wananchi wote kutumia fursa hiyo kumwezi Mheshimiwa Rais pamoja wa wanawake vinara katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wananchi.
Aidha, amesema katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani ni wajibu wa wanamorogoro wote kushiriki kikamilifu ili kuungana kwa pamoja kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu, huku wakitambua mchango wa wanawake na wasichana katika maendeleo ya Taifa letu.
"..Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kushiriki kwa wingi katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.." Amesema Mhe. Adam Malima.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema katika maadhimisho hayo ngazi ya Mkoa yataanza kufanyika Machi 6, 2025 ambapo kutakuwa na Shughuli za utalii, zitakazotoa fursa ya kujifunza na kuona vivutio vya utalii vilivyoko ndani ya mkoa huo na
Machi 7, 2025 kutakuwa na Kutoa msaada kwa wahitaji, Semina, Maonesho na Usiku wa Mwanamke.
Sanjari na hayo Mhe. Malima amesema kwa ngazi za Halmashauri maadhimisho hayo yataanza Machi 1- 5, 2025 ambapo yataambatana na matukio mbalimbali yakiwemo, Kuandaa mahojiano kuhusu nafasi ya mwanamke na mchango wake, kuandaa maonesho ya vikundi vya wanawake wajasiriamali, kuandaa makongamano yanayobeba ujumbe wa kauli mbiu, kuzindua afua/miradi mbalimbali ya kijamii na kutoa tuzo kwa wanawake vinara.
Shughuli nyingine zitakazofanyika wiki hiyo ni pamoja na kuandaa usiku wa mwanamke, kuendesha mashindano ya kitaaluma na michezo kutoa misaada ya kijamii kwa makundi ya wahitaji, kuandaa matembezi ya hiari na mashindano ya michezo, kuendesha kliniki ya msaada wa kisheria, bonanza la michezo kwa timu za wanawake na kushiriki kufanya shughuli mbalimbali za miradi ya kijamii.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima amewataka Wakuu wote wa Wilaya za Mkoa huo kusimamia kikamilifu maandalizi ya maadhimisho hayo na kuwahamasisha wananchi kushiriki shughuli zote zilizopangwa kufanyika kama ambavyo Wizara imeelekeza.
Katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kwa Mkoa wa Morogoro mgeni rasmi wa maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Mhe. Adam Kighoma Malima Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.