Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amesema, Wizara hiyo imedhamiria kutatua changamoto ya muda mrefu ya uhaba wa maji katika Manispaa ya Morogoro, kazi ambayo amesema itafanyika kwa ushirikiano na viongozi wa Mkoa huo na taasisi za maji, ili kuwapatia maji safi na salama wananchi wa Halmashauri hiyo pamoja na kushughulikia tatizo kubwa la upotevu wa maji.
Katibu Mkuu amebainisha hayo Julai 2, 2025, alipotembelea visima vya maji vilivyochimbwa katika eneo la Kayenzi, Kata ya Mafisa Manispaa ya Morogoro kujionea utekelezaji wa miradi ya maji ambapo pia alikutana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima pamoja na wataalamu wengine wa maji kujadili suala la upatikanaji wa maji katika Manispaa hiyo.
Mhandisi Mwajuma amesema, Mkoa huo una vyanzo vya maji vingi, hivyo Wizara imejipanga kwa dhati kushirikiana na Mkoa kuhakikisha maji yaliyopo ardhini yanatumika ipasavyo kupitia uchimbaji wa visima ili kutekeleza agizo la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhakikisha wananchi wa Morogoro wanapata maji safi na salama.
“Sisi kama Wizara ya Maji tutatekeleza maelekezo haya na wananchi wa Mkoa wa Morogoro waweze kupata huduma ya maji" amesema. Mhandisi Mwajuma Waziri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema kama uongozi wa Mkoa wamejizatiti kuhakikisha wananchi wa Manispaa ya Morogoro wanapata huduma ya maji huku akiweka wazi kuwa walianza na kazi ya kuunda kamati ya kutafuta vyanzo mbadala vya maji, hatua iliyowezesha kupatikana kwa maeneo ya kuchimba visima kama Mafisa na Tungi.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kayenzi, Bw. Mohamed Said ameishukuru Serikali ya Mkoa kwa kubuni njia za kutatua changamoto ya maji waliyokuwa wanaipata wananchi lakini zaidi amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea viongozi wanaojali wananchi na kushughulikia changamoto zao kwa vitendo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.