Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amemshauri Mkuu mpya wa Wilaya ya Mvomero, Maulid Hassan Dotto kufanya kazi zake kwa kutumia busara zaidi badala ya kutumia mabavu akifuata maadili ya uongozi huku akitambua lengo mahususi kuwa ni kuwafanya wananchi wa wilaya ya Mvomero waishi kwa amani na utulivu.
Mhe. Malima ametoa wito huo Juni 27, 2025, wakati wa hafla fupi ya kumwapisha Mkuu wa Wilaya huyo iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kufuatia uteuzi wa viongozi mbalimbali uliofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Juni 23 mwaka huu.
Mhe. Malima amesema, maamuzi ya busara ni bora zaidi kuliko maamuzi yale ya kutumia nguvu, mabavu na kutumia vyombo mbalimbali alivyokabidhiwa kumsaidia huku akimsisitiza kwenda kufanya kazi bila ubaguzi wa rangi, kabila au dini.
“Nakutakia kila la heri. Maamuzi mengi yanapaswa kufanywa kwa misingi ya busara kuliko kutumia mabavu,” amesisitiza Mhe. Adam Malima.
Katika hatua nyingine amemkumbusha Maulid Hassan kwamba hiki ni kipindi cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa Urais, wabunge na Madiwani, hivyo amemtaka kwenda kuimarisha hali ya ulinzi na usalama Wilayani humo ili uchaguzi ujao katika Wilaya hiyo ufanyike kwa Haki, Amani na Utulivu.
Naye katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa amemtaka kwenda kuendeleza mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake hususan programu ya TUTUNZANE ambayo imeleta matunda mema baina ya wakulima na wafugaji wa Wilaya ya Mvomero hivyo akaiimarishe ili makundi hayo yaendelee kuishi kwa amani kama ilivyo sasa.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Mashariki Selemani Shabani Selemani amemtaka Mkuu huyo wa Wilaya kuishi kwa kufuata kiapo cha maadili alichoweka leo huku akimtakia utekelezaji mwema wa majukumu yake.
Mhe. Maulid Hassan alipopewa fursa ya kusema neno, pamoja na kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa mapokezi yake mazuri, amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kumuamini huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Mvomero na Taifa kwa ujumla.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.