Waziri wa katiba na Sheria Mhe. Damas Ndumbaro ameagiza wananchi wa Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro kutumia kikamilifu Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia kutatua migogoro inayowakabili hususan migogoro ya kijiji cha Utengule, Kambenga na Namhala.
Mhe. Ndumbaro ametoa agiza hilo Disemba 14, Mwaka huu wakati akizindua kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia "Mama Samia Legal Aid Campaign" katika kijiji cha Mkamba Wilayani Kilombero Mkoani humo ikiwa ni siku ya kwanza tu mara baada ya kampeni hiyo kuzinduliwa Kimkoa Disemba, 13, 2024.
"...naomba nikuagize ester na timu yako katika ziara hii ambayo tupo hapa wilaya ya kilombero msiondoke bila kwenda kwenye hayo maeneo matatu yenye mgogoro muongee na pande zote mjue kiini cha mgogoro ni nini ikiwashinda tuleteeni sisi taarifa mawaziri..." amesema Mhe. Dkt. Ndumbaro
Sambamba na hayo Mhe. Damas Ndumbaro amesema hifadhi ni maeneo ya watanzania wote kwa maslahi mapana ya nchi hivyo wanaovamia kwa maslahi yao binafsi watachukuliwa hatua kali za kisheria huku akiwaonya Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji wanaochochea migogoro ya ardhi kwa kugawa maeneo hayo kiholela watafikishwa katika vyombo vya sheria na kupata adhabu wanayostahili.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo ametembelea gereza la Kiberege na kusikiliza kero mbalimbali kwa wafungwa 15 na mahabusu 2 na kuwaahidi wafungwa hao kuletewa katika gereza hilo mifumo ya kidijitali kwa ajili ya kuhudhuria kesi zao kwa wale wanaokata rufaa baada ya hukumu wakiwa hapo gerezani bila ya wao kufika mahakamani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Dastan Kyobya amebainisha migogoro iliyopo Wilayani humo kuwa ni pamoja na ile inayotokana na uvamizi wa misitu ya asili, migogoro ya ardhi, taraka, mirathi, mgawanyo wa mali na mashamba makubwa, mgogoro wa Kambenga, Mgogoro wa kijiji cha Namhala ambao hadi sasa una miaka 15 na mgogoro wa Kalenga kata ya Mofu.
Nao wananchi wa Kijiji cha Mkamba akiwemo Bi. Stamel Mlokota ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa maelekezo mahsusi na kuahidi kutekeleza kwa vitendo kampeni hiyo kwani amesema wananchi wa Wilaya hiyo wanakabiliwa na migogoro mingi ya ardhi, hivyo kampeni hiyo itawasaidia kutatua kero zao.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.