Madiwani Gairo watakiwa kusimamia mapato, miradi ya maendeleo
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro wametakiwa kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato yanayotokana na vyanzo mbalimbali vya ndani pamoja na kusimamia miradi ya Maendeleo inayotekelezwa ili Halmashauri hiyo iweze kutekeleza kazi zake kikamilifu pamoja na kuwahudumia wananchi.
Wito huo umetolewa Desemba 8 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare wakati wa kikao cha Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe akitoa hotuba kwa Wahe. madiwani wa Halmashauri ya Gairo
Mkuu huyo wa Wilaya amesema ili shughuli za Halmashauri hiyo ziweze kutekelezwa, sharti ziwepo fedha za kutosha za kuiendesha Halmashauri na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo moja ya kazi kubwa ya Wahe. madiwani ni kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.
Mbunge wa Jimbo la Gairo Mhe. Ahmed Shabiby (aliyesimama) akitoa nasaha wakati wa Baraza.
“ili shughuli za halmashauri ziweze kutekelezwa kikamilifu, ni sharti pawepo na fedha za kutosha kwa ajili uendeshaji wa Halmashauri na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. kupitia hitaji hilo, natoa wito kwenu kuhakikisha mnasimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani” alisema Mchembe.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Gairo Mhe. Rehel Nyangasi
Hata hivyo, amesema hana maana Madiwani hao watoke kwenda kukusanya mapato ya halmashauri la hasha bali wanatakiwa kusimamia watendaji kukusanya mapato hayo kwa mujibu wa sheria ndogo walizo walizokubaliana katika vikao halali kwa kuwa kazi ya kukusanya mapato ni ya watendaji.
Mhe. Mchembe amesema Halmashauri ya Gairo pamoja na kwamba kwa sasa imepanda katika kukusanya mapato ukilinganisha na hapo awali, bado halmashauri hiyo ni ya mwisho ukilinganisha na Halmashauri nyingine za Mkoa wa Morogoro hivyo jitihada zaidi zinahitajika.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Gairo Augustino Chazua ambaye alikuwa Mwenyekiti wa muda wa Mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani akionesha barua yenye mapendekezo ya Majina ya watakaochaguliwa kuwa Viongozi wa Halmashauri.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Madiwani kusimamia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na zaidi kuhakikisha wanasimami thamani ya fedha ya mradi husika inaonekana badala ya kusubiri viongozi wa Serikali au chama kutoka ngazi za juu wanapofanya ziara katika maeneo yao kuwalalamikia kuhusu miradi hiyo kutokuwa na ubora unaostahili.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Agnes Mkandya (wa tatu kulia) akijadili jambo na Mwenyekiti wa muda wa baraza la Madiwani pamoja na watendaji wengine
Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Gairo Mhe. Ahmed Shabiby aliyeshiriki kikao hicho, amewataka Madiwani wenzake kuelewa kuwa wamechaguliwa na wananchi kwa ajili ya kwenda kuisaidia Halmashauri ya Gairo kusonga mbele na kuwaletea wananchi maendeleo na si vinginevyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Gairo Mhe. Rehel Nyangasa akikabidhiwa moja ya vitendea kazi vya Kiti chake
Mapema kabla ya uchaguzi, akiomba kura za kurudi katika kiti cha Uenyekiti wa Halmashauri hiyo ya Gairo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Rahel Nyangasi ambaye tena amekalia kiti hicho amewataka Madiwani wenzake kusahau yote yaliyojitokeza kipindi cha mchakato wa uchaguzi na kusameheana huku akiwataka wote kufungua ukurasa mpya wa kuchapa kazi.
Watendaji kutoka Sekretarieti ya Mkoa wakiwa makini kufuatilia na kuhakikisha Baraza hilo linatekeleza agizo hilo kwa kufauata sheria na miongozo yote inayotakiwa
Mhe. Rahel Nyangasi alichaguliwa kwa kura 22 kati ya kura 24 za wajumbe waliokuwepo ukumbini na kupiga kura hivyo kuthibitishwa kuwa Mwenyekeiti wa Halmashauri ya Gairo huku Clemence Msulwa akishika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa kupigiwa kura 23 kati ya kura 25 zilizopigwa na wajumbe huku kura mbili zikiharibika.
Viongozo mbalimbali waliohudhuria wakati wa kikao cha Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Gairo Mkoani Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.