Mkoa wa Morogoro una mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 5,295.04 kama ifuatavyo:-
Jedwali Na. 93: Aina za Barabara
S/N
|
Aina ya Barabara
|
Urefu (Kilometa)
|
1
|
Barabara kuu
|
845.98 |
2
|
Barabara za Mkoa
|
1,048.06 |
3
|
Barabara za Wilaya
|
3,401.00 |
|
JUMLA
|
5,295.04 |
Mkoa wa Morogoro una miradi mikubwa ya Kitaifa inayotekelezwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Makao Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakala wa Barabara Mkoani.
Ujenzi wa Barabara ya Magole – Mziha (Magole – Turiani –Km 48.6)
Ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami unajumuisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa Km 45.2, madaraja mapya manne (4), Box culverts 17 na makalavati madogo 187 (concrete pipe culverts).
Ujenzi huu umefanywa na Kampuni ya Ujenzi ya M/s China Civil Engineering Construction Corporation Ltd (CCECC) kutoka China kwa gharama ya awali ya shilingi milioni 41,890.860 ambayo imeongezeka na kuwa shilingi milioni 66,717.702 bila VAT. Mkataba huu ulisainiwa tarehe 17 Juni, 2009 na kazi ilianza rasmi tarehe 03 Machi 2010. Muda wa awali wa kazi hii ulikuwa miezi 27 na mradi ulipangwa kukamilika tarehe 02 Juni 2012, Hata hivyo kazi hii haikukamilika kama ilivyopangwa kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo ya uhaba wa fedha na kuongezeka kwa kazi, hivyo Mkandarasi aliongezewa muda akamilishe mradi ifikapo tarehe 30 Octoba 2017. Kwa sasa Mradi huu umekamilika na Mkandarasi anafanya kazi ndogondogo za kumalizia mkataba wake.
Mhandisi Mshauri (Supervision Consultant) aliyesimamia mradi huu ni H.P GAUFF INGINIERE GmbH & CO. JBG CONSULTING ENGINEERS ya Ujerumani ikishirikiana na NIMETA CONSULT (T) LTD ya Tanzania. Jumla ya Mkataba wa Mhandisi Mshauri ni T.Shs. 6,874,393,600.31
Ujenzi wa Daraja la Kilombero
Serikali ya Tanzania ilisaini Mkataba wa Ujenzi wa Daraja la Kilombero na Mkandarasi M/s China Railway 15 Group Corporation kutoka China, tarehe 24 Oktoba, 2012. Mradi huu unahusisha ujenzi wa Daraja kubwa lenye urefu wa mita 384 na Daraja dogo la urefu wa mita 120, "Box Culverts" 31, makalvati 18 na maingilio ya barabara yenye jumla ya urefu wa Kilometa 9.142. Gharama ya mradi huu ni shilingi 53,214,395,756.87 bila VAT na umetekelezwa kwa kutumia fedha za ndani (Government of Tanzania Funds).
Mkandarasi alianza kazi rasmi tarehe 21 Januari, 2013 na muda wa kazi ulikuwa miezi 24, hivyo tarehe ya awali ya kukamilisha mradi ilikuwa 20 Januari, 2015 kabla ya kupewa muda wa nyongeza wa hadi tarehe 30 Septemba, 2016. Hata hivyo kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza likiwemo la uhaba wa fedha na mafuriko yaliyojitokeza mfululizo mwaka 2013, 2014 na 2015, Mradi haukukamilika kama ulivyopangwa Mkandarasi alipewa muda wa nyongeza tena hadi 30 Septemba 2017. Kwa sasa utekelezaji wa kazi hii umekamilika kwa asilimia 100.
Mhandisi Mshauri (Supervision Consultant) aliyesimamia mradi huu ni M/s AARVEE Associates Architects, Engineers & Consultants PVT Ltd ya kutoka Hyderabad, INDIA akishirikiana na Ms Advanced Engineering Solutions (T) Ltd, P.O. Box 19074, Dar es Salam, TANZANIA kwa gharama ya shilingi milioni 2,759,255,000.00.
Ujenzi wa barabara ya Dumila – Kilosa – Mikumi (km 142) kwa kiwango cha lami (sehemu ya Rudewa – Kilosa, km 24)
Katika mradi huu jumla ya km 24 kuanzia Rudewa hadi Kilosa mjini zitajengwa ili kuunganisha sehemu ya barabara ya Dumila – Rudewa (km 45) iliyokwishajengwa kwa kiwango cha lami. Jumla ya shilingi bilioni 11.838 zimeidhinishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 kwa ajili ya ujenzi. Kwa sasa taratibu za manunuzi kumpata Mkandarasi zinaendelea kwa ajili kazi ya ujenzi.
Ujenzi wa Barabara ya Mikumi - Kidatu – Ifakara (sehemu ya Kidatu – Ifakara, Km 66.9 pamoja na ujenzi wa Daraja la Ruaha Mkuu) kwa kiwango cha lami.
Mradi huu wa kujenga sehemu ya barabara kati ya Kidatu na Ifakara kwa kiwango cha lami (Km. 66.9) na Daraja la “Great Ruaha” umeshaanza chini ya udhamini wa muungano wa Ulaya (EDF) kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.
Mkataba wa Ujenzi wa barabara hii ulitiwa saini kati ya Serikali na Mkandarasi M/s Reynolds Construction Company kutoka Nigeria, tarehe 24 Julai, 2017. Mradi huu unahusisha ujenzi wa Daraja kubwa la mto Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 150, Madaraja mengine manne (4) yenye urefu wa mita 27 na 23, "Box Culverts" 36, makalvati madogo (Pipe Culvert) 266 na barabara yenye jumla ya urefu wa Kilometa 66.9.
Gharama ya mradi huu ni EURO 40,441,890.81 bila VAT. Mkandarasi alianza kazi rasmi tarehe 02 Oktoba, 2017 na muda wa kazi ni miezi 30, hivyo tarehe ya awali ya kukamilisha mradi ni tarehe 20 Machi, 2020
Mhandisi Mshauri (Supervision Consultant) anayesimamia mradi huu ni M/s Nicholas O'Dwyer and Co. Ltd kutoka nchi ya Ireland
Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri za Wilaya Mkoa wa Morogoro iliidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni 8,165,610,000 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na madaraja na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini umeidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni 8,851.13 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na madaraja.
Utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara na madaraja katika mwaka wa fedha 2016/2017 unaendelea na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 upo katika hatua ya manunuzi.
Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi mwenzi Juni 2017 Halmashauri za Wilaya zilipokea kiasi cha shilingi 3,998,166,378.95 ambayo ni sawa na asilimia 55.5 ya bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ya shilingi milioni 7,206.523. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 fedha zilizopokelewa ni shilingi 2,279,020,742.84 sawa asilimia 25.7 ya bajeti iliyoidhinishwa ya shilingi milioni 8,851.13.
Kazi ya utekelezaji wa Matengenezo ya barabara na madaraja kwa mwaka wa fedha 2016/2017 unaendelea na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 upo katika hatua ya manunuzi.
Kwa kipindi cha miaka mitatu ya fedha mfululizo yaani 2014/2015, 2015/2016 na 2016/2017 fedha za barabara zimekuwa hazifiki kwa wakati hii imepelekea kuathiri utekelezaji ,
Wakandarasi wazawa kuwa na mitaji midogo na kutokuwa na wataalamu hivyo kupunguza ufanisi katika utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara na madaraja.
Ujenzi wa Daraja la Mwere katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro umekamilika na umetumia gharama ya shilingi 1, 605, 107,655/=.
Ujenzi wa Daraja la chuma lenye urefu wa mita 39 umefanyika na kukamilika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero na kugharimu takribani shilingi 747,254, 351.99
Mkoa wa Morogoro katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inatekeleza mradi wa kuboresha miundombinu ya barabara chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia (World Bank) kupitia Programu yake ya kuimarisha Serikali za Mitaa nchini (Tanzania Urban Local Government Strengthening Program (ULGSP). Program hii inakusudia kuinua uwezo wa utoaji huduma katika Halimashauri nchini.
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri 18 za miji na Manispaa zinazotekeleza miradi ya uboreshaji miundombinu kupitia program ya “Urban Local Government Support Programme” (ULGSP). Katika kuboresha kuboresha miundombinu, Manispaa ya Morogoro inayo miradi miwili ya kuinua hadhi ya barabara zifuatazo:-
Barabara ya Mei Mosi
Ujenzi wa mradi huu ulihusisha barabara tatu za Mei mosi I, II na III zenye jumla ya urefu wa km 5.1. Kazi kubwa zilizofanyika ni:-
Kusafisha eneo la ujenzi
Kukata maeneo yaliyoinuka na kufukia maeneo mengine ili kupata usawa wa barabara
Kujenga box na pipe culverts
Kujenga matabaka ya chini ya barabara
Kuweka tabaka lililochanganywa na saruji
Kujenga tabaka mwamba uliosagwa na kuweka lami kianzio (prime coat)
Kuweka zege la lami nzito ya unene wa mm 50 (asphalt concrete)
Kuweka lami nyepesi kwenye sehemu ya waenda kwa miguu
Kujengea mifereji ya maji ya mvua
Kuweka taa za barabarani (solar street lights)
Ujenzi wa barabara ya Mei Mosi unatekelezwa na Mkandarasi Jassie & Company Limited kwa gharama ya 11,805,176,469.00. Kazi zilizoingiwa Mkataba ni:
Uwekaji wa tabaka la “base” kutumia mawe yaliyosagwa.
Uchimbaji na ujenzi wa mifereji.
Uwekaji wa tabaka la lami nzito (asphalt concrete).
Mkataba huu pia ulihusisha masuala ya:-
Afya na usalama
Utunzaji wa mazingira
Uondoaji wa miundombinu ikiwemo ya mabomba ya maji safi na maji taka ya MORUWASA (Tsh. 150,000,000); nguzo za TANESCO (Tsh. 51,530,166.71) na nyaya ukiwemo mkongo wa Taifa unaomilikiwa na TTCL (Tsh. 27,086,378.35).
Uondoaji wa muindombinu ulichelewa sana kwa kuchukua zaidi ya miezi sita hivyo kuchelewesha kazi za ujenzi wa barabara. Hali hii ilisababisha kuongeza muda wa kazi kwa Mkandarasi na Mhandisi mshauri.
Wakati kazi ya ujenzi ikiendelea, mabadiliko ya design ya barabara yalifanyika hatua ambayo iliokoa kiasi cha sh. 762,034,360 ambazo zitumika kujenga km 2 za barabara za lami nyepesi. Kazi ya ujenzi wa barabara hii imekamilika.
Barabara za Tubuyu, Nanenane na Maelewano
|
CHANGAMOTO |
Kumekuwa na changamoto kadhaa wakati wa utekelezaji; nitaje chache ambazo zimechelewesha utekelezaji na pia zimekuwa na tishio la kuongezeka kwa gharama.
Barabara ya Maelewano imekuwa na chemchem ya maji kutoka chini ya ardhi hivyo kusababishi ugumu wa kuandaa tabaka la kwanza kabla ya kuweka matabaka ya yanayofuata. Tumelazimika kuweka mifereji chini ya ardhi ili kukusanya maji hayo kwa ajili ya kupata sehemu ya kujenga kitako cha barabara. Mifereji hii imejengwa kutumia mawe na kitambaa maalum (geotextile material). Kazi hii imekamilika. Mabomba makubwa ya kusambaza maji safi yenye kipenyo cha mm 200 yalikuwa eneo la ujenzi wa barabara ya Maelewano, uondoaji wake ulichukua muda mrefu; kazi hii sasa imekamilika. Nguzo za umeme pia zilikuwa eneo la Ujenzi kwenye barabara zote, uondoaji wake ulichelewa sana. Meta 800 za barabara ya Nanenane zilikuwa na udongo wa mbuga (black cotton soil), na maji ya ardhini yalikuwa juu karibu na usawa wa barabara, baada ya kupima udongo kwenye (CML) kule DSM, tulilazimika kubadilisha ‘design’ kwa kulazimika kuchimba na kuondoa udongo huu 600 mm na kujaza udongo mzuri unaoweka kuhimili uzito ili barabara iweze kuwa ya kiwango stahili. Jambo hili lina ongezeko la gharama Tunatoa shukrani nyingi kwa kupata ufumbuzi wa suala la Msamaha wa VAT. |
Mkoa wa Morogoro unatekeleza Miradi mikubwa miwili ya uondoaji wa vikwazo katika barabara za Halmashauri. Miradi hii inatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero na Gairo kupitia ufadhili wa Serikali ya Uingereza chini ya shirika la maendeleo (DFID) ikiwa na lengo la kuboresha huduma ya usafirishaji na kuondoa vikwazo katika barabara hususuani ujenzi wa vivuko na madaraja.
Kwa upande wa Halmashauri ya Kilombero mradi huu unatekelezwa katika Barabara ya Chita-Merela. Mradi huu ulianza tarehe 29/11/2015 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 30/09/2017.
Kazi kubwa iliyofanyika ni ujenzi wa maboksi kalavati 23 na kuinua tuta katika barabara na kuweka changarawe barabara yenye urefu wa km 11.245. Mradi huu unatekelezwa na wakandarasi wawili. Mkandarasi M/s Taba Construction & Luqman Construction Ltd (JV) anatekeleza kwa kiasi cha shilingi 3,905,026,383.15, (Kilometa 5.6), pamoja na BECCO Ltd, (Kilometa 5.6).
Mkandarasi M/s Taba Construction & Luqman Construction Ltd (JV) aliongezewa muda hadi tarehe 27 Desemba 2017. Kufuatia Mkandarasi huyo kutokufanya kazi kwa mujibu wa Mkataba, mkataba wake na Halmashauri umesitishwa, na taratibu za kumpata Mkandarasi mpya zinaendelea.
Kipande kingine (kilometa 5.6) kiko chini ya Mkandarasi BECCO Ltd kwa kiasi cha shilingi 3,016,894,495.56. Mradi huu ulianza tarehe 06/09/2016 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 30/09/2017 na aliongezewa muda hadi trehe 27/12/2017. Hata hivyo mkandarasi huyo bado hajamaliza kazi na kwa hatua aliyofikia inategemewa kwamba kazi hiyo itakamilika mwezi huu wa Januari.
Kwa upande wa Halmashauri ya Gairo mradi huu unatekelezwa katika Barabara ya Chagongwe – Kumbulu kazi kubwa iliyofanyika ni ujenzi wa maboksi kalavati 5 makubwa na kujaza kifusi katika makalavati. Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi T.G.S Company kwa kiasi cha shilingi 2,275,461,057.92 na ulianza tarehe 02/12/2015 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 25/10/2017. Kwa sasa mradi huu umekamilika na Mkandarasi anafanya kazi ndogondogo za kumalizia.
Ujenzi wa Makazi ya Viongozi
Serikali kupitia OR-TAMISEMI imeingia Mkataba na Wakala wa Majengo (TBA) katika kusimamia na kujenga nyumba za viongozi katika Wilaya ya Gairo na Mvomero kwa gharama ya shilingi 1,210,487,915.30
Katika Wilaya ya Gairo ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala Wilaya na Watumishi Waandamizi wawili zinajengwa.
Hatua ilipofikia ni kama ifuatavyo;
Nyumba ya Mkuu wa Wilaya ipo katika hatua ya msingi tayari msingi umekamilika na nguzo kuinuliwa,
Nyumba ya Katibu Tawala Wilaya ipo katika hatua ya linta,
Nyumba mbili za Watumishi Waandamizi ,zipo katika hatua ya linta,
Katika Wilaya ya Mvomero zinajengwa nyumba mbili kwa ajili ya Watumishi Waandamizi, nyumba hizo zipo katika hatua ya linta.
Ujenzi kwa sasa umesimama kutokana na kukosekana kwa fedha za kukamilisha. Fedha iliyotumika hadi kufikia hatua hiyo ni kiasi cha shilingi milioni 250 ambazo zilitengwa katika bajeti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa mwaka wa fedha 2014/2015. Kiasi kilichobaki katika mkataba inatakiwa kulipwa na OR-TAMISEMI kupitia bajeti ya Wizara iliyotenga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za viongozi.
Ukarabati wa Ofisi na Nyumba za Viongozi
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 miradi yenye jumla shilingi 524,008,506.89 inatekelezwa. Miradi hiyo ni ya ukarabati wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kwa gharama ya shilingi 89,858,874.71, na umekamilika, Ukarabati wa Nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero ambao unategemea kugharimu shilingi 87,648,362.16, Ujenzi wa Uzio na ukarabati wa makazi ya Mkuu wa Mkoa kwa ghrama ya shilingi 89,740,790.00 ambao umekamilika, Ukamilishaji wa ujenzi wa Rest House Ulanga kwa gharama ya shilingi 148,532,288.95, na Ukarabati wa jengo la kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro kwa gharama ya shilingi 108,228,191.07. Kazi hizi zinatekelezwa na Wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Morogoro na kazi zipo katika hatua mbalimbali za umaliziaji.
Pia kulikuwa na ununuzi wa majokofu yanayoweza kuhifadhi miili 18 kwa kwa wakati mmoja kwa kiasi cha shilingi milioni 61.2
SEKTA YA ARDHI
Hali ya ongezeko la watu na shughuli zao mbalimbali juu ya ardhi ambayo haiongezeki, imechangia kuongezeka kwa mahitaji zaidi ya ardhi na kuzua migogoro mingi ya wakulima na wafugaji, uharibifu wa mazingira, vyanzo vya maji pamoja na kujitokeza kwa ujenzi holela katika maeneo mbalimbali.
Hali hii imepelekea kuwepo kwa mahitaji makubwa ya upimaji wa ardhi, upimaji wa mipaka ya vijiji pamoja na mahitaji ya kuandaliwa kwa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ya Vijiji.
Upimaji wa Mipaka ya vijiji
Jumla ya vijiji 561 vimepimwa kati ya vijiji 659 vya Mkoa wa Morogoro. Idadi hii ya vijiji vilivyopimwa ni sawa na asilimia 85.12 ya vijiji vyote vya Mkoa wa Morogoro. Juhudi za makusudi zinafanyika ili kuhakikisha kwamba vijiji 98 vilivyobakia vinapimwa, kupewa vyeti pamoja na kuandaliwa mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi.
Uandaaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi
Mpaka sasa, vijiji 248 vimeandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kati ya vijiji 659. Idadi hii ya vijiji vyenye Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ni 248, sawa na asilimia 37.63.
Tunatambua kwamba idadi hii ni ndogo sana, na juhudi za makusudi zinatakiwa kuchukuliwa na Mkoa, Halmashauri pamoja na wadau wengine, ili kuhakikisha kwamba vijiji vingi vinaandaliwa mipango hiyo ili kuwawezesha wananchi vijijini kujikwamua kiuchumi, kuboresha mazingira pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji.
Tumezisisitiza Halmashauri kutenga fedha kwenye bajeti zao ili kuwezesha kuandaa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi wa angalau kijiji kimoja kila mwaka.
Uandaaji wa Hatimiliki za Kimila
Jumla ya Hati miliki za Kimila 19,552, zimeandaliwa katika Mkoa wa Morogoro.
Changamoto Katika Utendaji kazi
Uhaba wa Vitendea kazi
Vifaa vya Upimaji ardhi katika Halmashauri havitoshelezi, na hivyo kutokidhi kasi ya upimaji. Kunahitajika vifaa vya upimaji Ardhi vya kisasa na vya kutosha ili kuendana na kasi ya upimaji wa ardhi na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.
Ili kuweza kupima viwanja vingi kwa ufasaha na kwa muda mfupi, Kila Halmashauri inahitajika kuwa na angalau mashine ya upimaji (Total station) moja pamoja na RTK GPS moja. Hakuna hata Halmashauri moja yenye RTK GPS katika Mkoa. Halmashauri zenye Total Station moja kila moja ni tatu tu, ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mvomero na Kilombero.
Kugawanywa kwa vijiji
Mara nyingi, inapofikia wakati wa uchaguzi wa Serikali za vijiji, baadhi ya vijiji hupendekezwa kugawanywa na kuwa vijiji viwili au zaidi. Ugawanyaji wa vijiji unapofanyika huathiri mipango ya matumizi iliyoandaliwa.
Hali ya Migogoro ya Ardhi katika Mkoa
Hali ya ongezeko la watu na shughuli zao mbalimbali juu ya ardhi ambayo haiongezeki, imechangia kuongezeka kwa mahitaji zaidi ya ardhi na kuzua migogoro mingi ya wakulima na wafugaji, uharibifu wa mazingira, vyanzo vya maji pamoja na kujitokeza kwa ujenzi holela katika maeneo mbalimbali.
Aina ya migogoro ya Ardhi iliyopo katika mkoa
Kuna migogoro ya mbalimbali ya Ardhi iliyoripotiwa katika makundi yafuatayo:
i. Migogoro ya mipaka ya vijiji
ii. Migogoro Mipaka ya vijiji na taasisi
iii. Migogoro ya mipaka ya wilaya
iv. Migogoro ya mipaka ya mikoa
v. Migogoro Mikubwa kuhusu Milki za viwanja
vi. Migogoro Mikubwa kuhusu Miliki za Mashamba
vii. Migogoro ya wakulima na wafugaji
viii. Migogoro kati ya vijiji na maeneo ya hifadhi
Miongoni mwa migogoro ya mipaka ya vijiji iliyobainishwa hapo juu, ni migogoro mikubwa miwili ya wakulima na wafugaji katika vijiji vya Mabwegere na Kambala. Kuna hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhakikisha kwamba ufumbuzi wa kudumu wa migogoro hii miwili ya Ardhi unapatikana.
Chanzo cha Mgogoro wa kijiji cha Kambala.
Chanzo cha mgogoro wa kijiji cha Kambala na vijiji jirani ni kugombea rasilimali Ardhi pamoja na maji katika Bonde la Mgongola. Tatizo kubwa la mgogoro ni matumizi ya Bonde la Mgongola lenye ukubwa wa hekta 3,620.
Kwa ujumla, mgogoro wa Bonde la Mgongola umesababishwa na matatizo yafuatayo:
a. Kuwepo kwa mahitaji makubwa ya ardhi kwa shughuli za kilimo na ufugaji ikilinganishwa na ardhi iliyopo,
b. Uingiaji wa mifugo mingi kwenye bonde hilo kutoka ndani na nje ya wilaya
c. Uhaba wa miundombinu kwa ajili ya mifugo kama vile malambo na majosho.
d. Kutokuwepo kwa uadilifu miongoni mwa viongozi wa kata na vijiji kwa kuuza ardhi bila utaratibu.
e. Mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha uhaba wa malisho na maji kwa ajili ya mifugo.
f. Mabadiliko katika umiliki na Upimaji wa kijiji cha Kambala
Mgogoro wa kijiji cha Mabwegere
Kumekuwepo na mgogoro wa muda mrefu kuhusu hadhi na mipaka ya Kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani vya Mfulu, Mbigiri, Dumila Mambegwa na Matongolo.
Awali, kijiji cha Mabwegere kilikuwa kitongoji cha Mfulu. Kijiji Mama cha Mfulu kilisajiliwa na Mkurugenzi wa Maendeleo wa wilaya ya Kilosa tarehe 09 Februari 1976 kwa Hati Na. MG. KIJ.110.
Chanzo cha mgogoro
Kijiji cha Mabwegere kilisajiliwa na Msajili wa vijiji chini ya kifungu Na. 22 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Na. 7 ya mwaka 1982 tarehe 16 Juni 1999 kwa Hati Na. MG/KIJ.522, miaka 9 baada ya kijiji hicho kupata Hati ya kumiliki Ardhi ya Kijiji.
Halmashauri ya Kijiji cha Mabwegere ilipewa Hati ya Kumiliki Ardhi kama Kijiji mwaka 1990 wakati Kijiji kiliandikishwa mwaka 1999 yaani miaka tisa baadaye
Vijiji jirani vinakituhumu kijiji cha Mabwegere kumega maeneo ya vijiji vyao kupitia upimaji uliofanyika mwaka 1989 ambao haukuvishirikisha vijiji hivyo, na hivyo kuibuka kwa mapigano ya mara kwa mara baina ya jamii ya wafugaji na wakulima.
Aidha, inadaiwa kuwa uainishwaji wa mipaka ya kijiji cha Mabwegere haukuhusisha kikamilifu vijiji jirani vya Mambegwa, Dumila, Mfulu na Mbigiri, na hivyo kupelekea kijiji hicho kuwa ndani ya kata tatu tofauti. Kijiji hicho kimo ndani ya mipaka ya kata za Msowero (Kitongoji cha Kikenge), Mbigiri (Kitongoji cha Matangani) na Kitete.
Kwa upande mwingine, Serikali ya kijiji cha Mabwegere imekuwa ikivituhumu vijiji jirani kwamba viongozi wa vijiji hivyo hugawa ardhi ya kijiji cha Mabwegere kwa watu kutoka nje, hususan kutoka Morogoro na Dar es salaam, wakati ambapo kijiji hicho kimesajiliwa na kutakiwa kuwa na maamuzi yake kamili kuhusu ardhi yake.
Katika kushughulikia mgogoro wa Kijiji cha Mabwegere na Vijiji jirani vya Mambegwa, Mfulu, Mbigiri, Dumila, Mateteni na Matongolo; hatua zifuatazo zilichukuliwa:
(a) Baada ya Mhe. Mkuu wa Mkoa kumwandikia Waziri wa Ardhi, ili taratibu kwa mujibu wa Fungu la 7 (2) (a) la Sheria ya Ardhi Na. 5 ya mwaka 1999 ziweze kufanyika, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alimteua Msuluhishi wa Mgogoro huo ambaye tayari amefanya kazi hiyo, na kukabidhi taarifa kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tarehe 23 Februari, 2016.
(b) Baada ya Msuluhishi kufanya kazi yake na baada ya mgogoro huo kutokufikia mwafaka, aliiwasilisha taarifa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye kwa mamlaka aliyopewa chini ya Fungu la 18 la Sheria ya Ardhi Na. 4 ya Mwaka 1999, alimteua Mchunguzi wa mgogoro huo.
(c) Mchunguzi (Mhe.Jaji wa Mahakama Kuu Jacob Mwambegele) aliifanya kazi hiyo na kuikabidhi Serikalini. Kwa sasa yanasubiriwa maelekezo kutoka Serikalini ya namna ya kuutatua mgogoro huo.
Hatua zilizochukuliwa na Mkoa
Kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi
Mkoa umezihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi. Mpaka sasa, vijiji 268 vimeandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kati ya vijiji 659 sawa na asilimia 40.3.
Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliyoandaliwa kwa kila wilaya ni kama ifuatavyo:
- Wilaya ya Kilombero 69
- Wilaya ya Morogoro 49
- Wilaya ya Kilosa 37
- Wilaya ya Mvomero 74
- Wilaya ya Ulanga 34
- Wilaya ya Malinyi 05
Tunatambua kwamba idadi hii ni ndogo sana, hivyo juhudi za makusudi zinachukuliwa na Mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri pamoja na wadau wengine, kuhakikisha kwamba vijiji vingi vinaandaliwa mipango hiyo ili kuwawezesha wananchi vijijini kujikwamua kiuchumi, kuboresha mazingira pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji.
Mkoa umezielekeza wilaya zote kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji ikiwa ni pamoja na wafugaji kuchangia ujenzi wa miundombinu, hasa uchimbaji wa Marambo ya maji;
Mkoa umezielekeza Halmashauri zote katika Mkoa, kutunga Sheria Ndogo zinazohusu uimarishaji wa nyanda za malisho na udhibiti wa mifugo.
Kamati za Wafugaji na Wakulima zimeundwa katika ngazi za kata na vijiji ili kusaidia kutatua migogoro inayojitokeza katika ngazi hizo;
Halmashauri zimehimizwa kutoa Elimu ya Sheria ya Ardhi ya vijiji Na.5 ya mwaka 1999.
Serikali imewajengea uwezo wafugaji wa jamii ya Kimasai na kisukuma wanaoishi katika maeneo hifadhi oevu na maeneo mengine yaliyotengwa kwa hifadhi ya mazingira ili waweze kubadilisha mfumo wao wa ufugaji wa asili. Aidha, wafugaji katika wilaya ya Kilosa walikwenda Botswana na Kenya kujifunza mbinu za ufugaji wa kisasa;
Serikali imetoa Tamko la Kuzuia uingizaji holela wa mifugo kutoka nje ya mkoa wa Morogoro.
Kutokana na mkoa kuwa na mifugo mingi kuliko uwezo wa maeneo ya malisho, Mkuu wa Mkoa amekwishatoa tamko la zuio la uingizaji holela wa mifugo katika Mkoa mnamo tarehe 20 Mei,2016, ambapo Halmashauri za Mkoa wa Morogoro zimeagizwa kusimamia kikamilifu sheria na kanuni za mifugo katika uhamishaji wa mifugo kutoka eneo moja hadi lingine.
Serikali inasimamia Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji mifugo
Ili kudhibiti uingizaji holela wa mifugo kutoka nje ya mkoa wa Morogoro, Mkoa umeamua kusimamia utekelezaji wa Sheria Namba 12 ya mwaka 2010 inayohusu Usajili, Utambuzi na Ufuatiliaji wa mifugo kwa kuweka alama katika Ng’ombe wote walioko ndani ya Mkoa.
Shughuli zilizofanyika katika kutekeleza zoezi hilo kwa ngazi ya Mkoa ni pamoja na;
i. Kutoa maelekezo sahihi kwa Halmashauri kutekeleza zoezi hilo kwa ufanisi
ii. Kufanya vikao vya kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kwa ajili ya kuwashirikisha katika utekelezaji wa zoezi hilo
iii. Kufanya vikao na Watendaji wa Halmashauri zote katika mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kutoa Elimu stahiki kuhusu utekelezaji wa zoezi hilo, na
iv. Kufanya vikao na Chama cha Wafugaji ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya zote za mkoa wa Morogoro kwa lengo la kuwapa uelewa juu ya umuhimu wa zoezi hilo.
Aidha katika ngazi ya Halmashauri shughuli zilizofanyika ni pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu zoezi la Utambuzi wa mifugo kwa njia ya mikutano ya hadhara katika maeneo yao. Aidha baadhi ya Halmashauri zinaendelea na usajili wa Wafugaji na kupiga chapa ya moto katika mifugo.
Kila mfugaji anayesajiliwa anapewa kitambulisho cha kumtambua kuwa ni mfugaji halali wa mkoa wa Morogoro. Hadi kufikia tarehe 15 Januari 2018, jumla ya Ng’ombe 699,042 wamepigwa chapa ya moto kati ya ng’ombe 740,246 waliokusudiwa, sawa na asilimia 94 ya lengo.
Kuwasaidia wafugaji kupata soko la ng’ombe
• Mkoa umefanya mawasiliano na wawekezaji katika kiwanda cha nyama cha Nguru kilichopo wilaya ya Mvomero Morogoro ili watakapoanza uzalishaji waweze kununua mifugo kwa wafugaji kwa bei nzuri. Aidha baadhi ya Halmashauri kama vile Kilombero wameshafanya mawasiliano na Bodi ya Nyama ili kuwasaidia kutafuta soko la nje ya Nchi.
• Kuomba maeneo ya ranchi za mifugo za Taifa ambayo hayaendelezwa kupatiwa wafugaji.
• Mkoa umeomba kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kupatiwa eneo lenye ukubwa wa hekta 16,989 kwa ajili ya mifugo 6,795 katika Ranchi ya Mkata.
• Kutoa elimu kwa wafugaji juu ya ufugaji wenye tija, uvunaji wa mifugo na upandaji wa malisho
Mkoa umeziagiza Halmashauri zote ndani ya Mkoa kuwaelimisha wafugaji kufanya ufugaji wenye tija kwa kufanya yafuatayo;
a. Kuvuna mifugo ili wawekeze katika shughuli zingine za kiuchumi
b. Wafugaji kufuga idadi ya mifugo kulingana na uwezo wa eneo la malisho
c. Wafugaji kusitawisha malisho kwa ajili ya mifugo yao.
d. Wafugaji wenye uwezo kuwekeza katika uzalishaji wa malisho ya mifugo kibiashara
Serikali imeanzisha Mpango wa kupima na kumilikisha maeneo
Katika lengo la kukabiliana na migogoro ya Ardhi, Serikali imeanzisha Mpango wa Upimaji na Umilikishaji wa maeneo (Land Tenure Support Programme) unaotekelezwa katika Wilaya za Ulanga, Kilombero na Malinyi.
Mpango huo wa miaka mitatu ulioanza mwaka 2016 unahusisha upimaji wa Mipaka ya vijiji, uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya, Uandaaji wa mipango ya Matumizi ya Ardhi ya vijiji pamoja na Umilikishaji wa Ardhi kupitia Hatimiliki za Kimila.
Hadi kufikia Desemba 2017, Mpango huo umeweza kupima mipaka ya vijiji 73 katika wilaya za Kilombero (28), Ulanga (23) na Malinyi (22).
Kati ya vijiji 266 vilivyoandaliwa mipango ya matumizi ya Ardhi katika Mkoa, vijiji 41 vimeandaliwa chini ya Mpango huu katika wilaya za Kilombero (18), Ulanga (18) na Malinyi (05).
Aidha, Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya za Ulanga, Kilombero na Malinyi imeandaliwa na kuridhiwa na Halmashauri za wilaya husika.
Katika kipindi cha kuishia Desemba 2017, mashamba 48,929 yamepimwa katika vijiji 29, na Hatimiliki za kimila 10,552 zimeandaliwa katika wilaya za Kilombero (9,312) na Ulanga (1,240).
Kuhimiza ufugaji wa kibiashara na wakisasa.
Serikali imekuwa ikihimiza ufugaji wa kisasa na kibiashara hususan katika ranchi za vikundi na wafugaji binafsi. Ufugaji wa aina hii hurahisisha kutumia teknolojia mpya na mbinu za kisasa kupata mifugo bora. Hii humwezesha mfugaji kuwa na mifugo michache iliyo bora, yenye tija na kuondoa haja ya kuwa na idadi kubwa ya mifugo inayoharibu mazingira na kusababisha migogoro ya ardhi.
Kubuni na Kutekeleza miradi ya kukarabati Rasilimali Ardhi.
Serikali ilibuni na kutekeleza miradi ya kuboresha rasilimali za ufugaji ikiwemo ardhi, nyanda za malisho na miundombinu. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa uendelezaji nyanda za malisho Masaini ambao ulilenga kuboresha mifugo na nyanda za malisho kwa kuweka miundombinu muhimu ya uzalishaji na masoko katika maeneo ya ufugaji
Namna tunavyoendelea kukabiliana na changamoto ya Migogoro ya ardhi
Katika kukabiliana na changamoto hii ya migogoro ya ardhi, hususan migogoro ya wakulima na wafugaji, Mkoa unaendelea kuchukua hatua zifuatazo:
1. Kuzihimiza Halmashauri za Wilaya kutenga Bajeti kwa ajili ya kuandaa Mipango ya matumizi bora ya Ardhi katika vijiji vilivyobakia angalau vijiji 5 kwa kila mwaka.
2. uwahimiza wafugaji ili waimarishe nyanda za malisho, ikiwa ni pamoja na kuweka padocks, katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ufugaji ili mifugo mingi iweze kutumia maeneo madogo madogo kwa mzunguko, badala ya mtindo wa sasa wa uchungaji holela wa mifugo unaoharibu mazingira na kusababisha migogoro ya Ardhi.
3. Kuwahimiza wafugaji kuweka miundombinu ya maji na majosho katika maeneo yao ya ufugaji.
4. Kuwaelimisha wafugaji kwa vitendo kuhusu kilimo cha malisho ya mifugo na kuanza kufuga kwa tija na kuacha uchungaji wa holela, kuvuna mifugo ili wabaki na kiasi cha mifugo kinachoendana na eneo la malisho.
5. Kuhakikisha kwamba kila Mpango wa matumizi bora ya Ardhi unakuwa na Sheria ndogo zilizoridhiwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji pamoja na Halmashauri ya wilaya husika.
Mashamba yaliyotelekezwa
Mkoa wa Morogoro una mashamba makubwa yaliyokaguliwa 311, ambapo mashamba 9 yamewasilishwa kwa Kamishna wa Ardhi kwa ajili ya kupendekeza kufutwa, mashamba 86 yametolewa ilani. Orodha ya mashamba hayo kwa kila wilaya ni kama ifuatavyo:
i. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuna mashamba pori 26, ambapo mashamba yote 26 yametolewa ilani ya uendelezaji, na tayari mashamba matatu yamefutwa.
ii. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mashamba 46 yametolewa ilani, mashamba 3 kuwasilishwa Wizara ya Ardhi kwa ajili ya kufutwa, na mashamba 11 yamefutwa rasmi. Mashamba yaliyofutwa yameshatayarishiwa Mpango wa kuyagawa upya.
iii. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero mashamba 17 yamekaguliwa, na shamba moja limefutwa.
iv. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mashamba 183 yamekaguliwa, 20 yametolewa Notisi na mashamba 6 yamewasilishwa Wizara ya Ardhi kwa ajili ya kufutwa. Katika wilaya ya Kilosa, mshamba 11 yamefutwa katika kipindi cha mwaka 1983 – 2017.
Kwa ujumla, mashamba yaliyofutwa kwa mkoa mzima katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2017 ni 30.
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.