Mkoa wa Morogoro uko mafichoni kwa sasa kwa ajili ya kujitathmini na kuweka mpango mkakati wa kurudisha heshima ya Mkoa huo kuitwa ghala la Taifa ili jina hilo litafisiliwe kwa vitendo zaidi.
Hayo yamebainishwa Februari 15 mwaka huu na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo wakati akifungua kikao cha kuhuisha mpango mkakati wa maendeleo wa sekretarieti na mamlaka ya serikali za mitaa kinachoendelea kufanyika Mkoani humo.
Mhandisi kalobelo amesema bado anaendelea kujiuliza swali ambalo Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa akijiuliza mara nyingi sababu ya Tanzania kuwa maskini ilhali ina utajiri wa kutosha, hali kadhalika amesema Morogoro ni moja ya mikoa hapa nchini yenye utajiri wa kila aina haoini sababu ya kuwa maskini.
Amesema haoni sababu ya Mkoa kuendelea kuimba kuwa ghala la taifa bila kuona manufaa yake wala uhalisia wa kaulimbiu hiyo, hivyo amewataka wadau wa kikao hicho wanaoendelea kuandaa Mpango mkakati wa maendeleo wa sekretarieti na mamlaka ya serikali za mitaa kinachoendelea kufanyika Mkoani humo kurejesha kwa vitendo kauli hiyo.
“Mpango Mkakati huu utuambie kwa sababu tuna ardhi nzuri ya Kilimo, basi tunataka mwaka huu zao Fulani lisipungue kiasi hiki na ndani ya miaka mitano uzalishaji wetu ufikie huku” alisisitiza Mhandisi Kalobelo.
Katika kikao hicho ambacho kinafanyika katika ukumbi wa Elimu ya Watu Wazima (WAMO) Mhandisi Kalobelo aligusia namna Mkoa unayvotakiwa kujiandaa kutangaza masuala ya Utalii, na vivutio vyote vilivyoko ndani ya Mkoa huo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Anza - Amen Ndossa amesema bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano 2021-2022 hadi 2025-2026 Mkoa unalazimika kuutafsiri mpango huo kikamilifu kwenye mipango ya maendeleo ya Mkoa na mamlaka ya Serikali za mitaa.
Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Cosmas Ngangaji amebainisha kuwa mpango Mkakati huo unaoandaliwa utasaidia kuweka shabaha zitakazotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano huku matarajio makubwa ni kuwa na uchumi shindani unaoongozwa na mazao yanayotokana na viwanda kwa maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro.
Naye Mshiriki wa wa Mpango mkakati huo Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Morogoro Janeth Balongo amesema hatua hii ya kutekeleza mpango mkakati sekta ya Elimu inatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi – CCM kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza hadi cha nne na kuendelea na ngazi zingine za Elimu ikiwemo Chuo kikuu.
Mpango Mkakati ni nyaraka muhimu ambayo inaoonesha dira ya taasisi kwa miaka mitano ijayo. Uwepo wa mpango huo utaongeza uwajibikaji wa utendaji kazi kuanzia ngazi ya taasisi, Idara, vitengo hadi ngazi ya mtumishi.
Mpango Mkakati huo utaleta uwazi na kuboresha mawasiliano kati ya menejimenti watumishi na wadau wengine wa maendeleo na kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wananchi.
Mpango Mkakati huo una maudhui yasemayo Kujenga uchumi shindani, unaoongozwa na mauzo ya nje na pia utasaidia upangaji mzuri wa rasilimali kwa kuzingatia vipaumbele vya taasisi, lengo kuu la Mpango huo ni kutekeleza mpango mkakati wa Taifa awamu ya tatu.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.