Mkuu Wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani humo kuchunguza ubadhilifu wa fedha za mradi wa ujenzi wa Mabweni mawili ya wasichana na bwalo la chakula katika shule ya Sekondari ya Gairo.
Loata Sanare ametoa agizo hilo Januari 24 mwaka huu wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Gailo alipotembelea Shuleni hapo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule hiyo.
Loata Sanare amesema hakuna sababu yoyote ya msingi ambayo imepelekea kutokamilika kwa ujenzi huo kwa kuwa Serikali imepeleka Shilingi 260 Mil. Kwa ajili ya ujenzi huo ambapo shilingi milioni 160 ni kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili na shilingi milioni 100 kwa ajili ya bwalo la chakula.
Katika hatua nyingine, Loata Sanare ametoa wiki moja kwa TAKUKURU kufanya uchunguzi wa mradi huo na kuwasilisha taarifa yake katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kabla au ifikapo Januari 29 mwaka huu ili kuwachukulia hatua wale watakaobainika kufanya ubadhilifu wa matumizi ya fedha hizo za umma.
Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo amewasimamisha kazi wataalam wa ujenzi wa mradi huo na kumuagiza kamanda wa jeshi la Polisi Wilaya ya Gairo (OCD) kumshikiria Mkandarasi Izengo Majija ambaye anahusika na usimamizi wa ujenzi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU Mkoani hapa Janeth Machulya amebainisha kuwa hadi sasa uchunguzi umeanza kufanyika ili kubaini matumizi yasiyo halali ya fedha hizo, kisha watawasilisha taarifa ya uchunguzi huobaada ya kukamilika.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Gairo Zainab Yambi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa Shule hiyo, amesema kamati yake ilikuwa ikihusika na kupitisha vifaa vinavyohitajika kutoka kwa wataalam wa ujenzi kisha kufikisha mahitaji hayo kwenye kamati ya manunuzi na baada ya manunuzi kuwasilisha vifaa hivyo kwa wataalam hao kwa ajili ya kuendelea na kazi.
Ujenzi wa mradi wa mabweni mawili ya wasichana na bwalo moja la chakula ulianza Julai 2020 na ulitakiwa kuamilika Oktoba 2020, hata hivyo hadi sasa ujenzi huo umefanyika kwa asilimia 40 tu licha ya Serikali kupeleka shilingi 260 Mil. kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.