Halmashauri za Mkoa wa Morogoro zimetakiwa kujifunza mbinu za ufundishaji ambazo zimetumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi kuwafundisha wanafunzi nakufanikisha kushika nafasi ya kwanza Kimkoa na ya tisa kitaifa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2020.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare katika hafla iliyofanyika Februari 23 mwaka huu kwa ajili ya kuzipongeza shule zilizofanya vizuri Wilayani humo katika matokeo ya mitihani ya darasa la saba ya mwaka 2020.
‘’Lakini nawahakikishia mmenipa jambo la kuzungumza, kila ninapopita nawambia nendeni mkajifunze kule Malinyi, nyinyi watu wa Manispaa nyie watu mnaokaa karibu na Manispaa mmeshindwa na watu wanaoitwa wa porini’’ amesema Sanare.
Aidha, Loata Sanate ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kuupa heshima Mkoa wa Morogoro na kuufanya kutambulika, licha ya changamoto mbalimbali za kielimu zilizokuwepo bado Halmashauri hii ya Malinyi imeibuka kuwa ya kwanza na kuzishinda Halmashauri nyingine za Mkoa huo.
Hata hivyo, Loata Sanare ametoa wito kwa Halmashauri hiyo kuongeza jitihada katika ufundishaji ili waweze kubaki katika nafasi hiyo ya kwanza huku akiwasisitiza kutobweteka kutokana na kushika nafasi hiyo badala yake wajipange vizuri ili mwakani waweze kutetea nafasi yao.
Awali, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa Loata Ole Sanare, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Masele amesema Halmashauri hiyo itaendelea kufanya vizuri kama ambavyo imefanya mwaka jana na kuendelea kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinaikumba sekta ya Elimu katika Halmashauri hiyo ili zisiwe kikwazo kwa matokeo yajayo.
Akibainisha mpango mkakati wa kuendeleza kufanya vizuri katika Sekta ya Elimu, Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Bi. Linda Malandu amesema, Halmashauri hiyo imejipanga kudhibiti utoro kwa wanafunzi, kuhamasisha walimu kujiendeleza kitaaluma na kuendelea kuhimiza wazazi kuhusu uchangiaji wa chakula kwa wanafunzi ili waweze kupokea maarifa vizuri wawapo darasani.
Akizungumzia changamoto zinazoikumba Halmashauri hiyo katika Upande wa Elimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Bi. Hawa Mposi amesema Halmashauri hiyo ina upungufu wa walimu 417 kati ya 800 wanaohitajika Wilayani humo.
Mkoa wa Morogoro umeshika nafasi ya nane kitaifa katika matokeo ya mtihani wa Taifa darasa la saba mwaka 2020, huku Halmashauri ya wilaya ya Malinyi imeshika nafasi ya kwanza kimkoa kati ya Halmashauri tisa za mkoa huo sawa na asilimia 96 za ufaulu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.