Wananchi hususan wajasiliamali wadogo Mkoani Morogoro wameendelea kunufaika na Mradi wa ufugaji kuku wanaostahimili magonjwa unaoendeshwa na Mradi wa Lishe Endelevu na kufadhiliwa na shirika la Misaada ya Kimataifa kutoka Marekani (USAID) hivyo kuendelea kukuza uchumi wao
Hayo yamethibitika Disemba 10, 2020 wakati Meneja wa Mradi wa Lishe Endelevu Mkoa wa Morogoro Bw. Nuhu Yahya, alipokuwa anakabidhi kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo Vifaranga vya Kuku 800 kwa ajili ya wanavikundi wa Wilayani Kilosa kwa ajili kuwapatia wakulima au wafugaji wa mfano ambao wataendelea kutoa mafunzo kwa akina Mama wanaowazunguka.
Bw. Yahya amesema wakulima au wafugaji hao wa mfano watapata vifaranga 200 na baada ya mwezi mmoja mfugaji atatakiwa kutoa robo tatu ya vifaranga hivyo kwa vikundi malezi vya kinaMama ambavyo vinapata mafunzo kutoka Mradi huo wa Lishe Endelevu.
kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewaagiza Wakurugenzi na Maafisa Ugani Mkoani humo kutoa ushirikiano katika mradi huo ili kufikia malengo ya Serikali katika mipango yake ya kuimarisha Lishe bora kwa wananchi.
Mhandisi Kalobelo amesema mradi huo unalenga kuisaidia serikali katika mipango ya kuimarisha Lishe bora kwa wanawake wenye umri wa uzazi na Kupunguza Udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Aidha, amesema licha ya mradi huo kupunguza udumavu kwa watoto hao, unakuza shughuli za kiuchumi katika jamii ikiwa ni pamoja na kuongeza kipato hivyo kuwataka wananchi watakaonufaika na mradi huo kuutunza kikamilifu msaada watakaopewa.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Kalobelo ametumia nafasi hiyo kumuagiza Mkuu wa Idara ya Uchumi wa sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro, kuongeza uratibu wa programu ya mradi huo katika kutambua Maafisa Ugani katika kata na Halmashauri namna wanavyo jishughulisha na uendelevu wa programu hiyo.
Naye, Afisa Kilimo na Mifugo wa shirika la lishe endelevu Agnes January, amesema Jamii imeupokea mradi huo kwa mwitikio chanya kutokana na elimu ambayo wameitoa juu ya faida zinazotokana na Ufugaji wa vifaranga hivyo.
Mradi wa USAID Lishe Endelevu hapa nchini umeanza rasmi mwaka 2018 na kuzinduliwa rasmi Mei 30, 2019 Mkoani Rukwa na Mhe. Selemani Jafo Waziri katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Mradi huu unaofadhiliwa na Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani (USAID) ni wa miaka minne na unalenga kuisaidia serikali katika mipango ya kuimarisha Lishe bora kwa wanawake wenye umri wa uzazi kuanzia miaka 15 hadi 49, kupunguza udumavu kwa asilimia 15 kwa watoto walio chini ya miaka mitano ifikapo mwaka 2022, na kuwaandaa wasichana 330,000 wa umri wa kubalehe.
Kwa sasa Mradi wa Lishe Endelevu katika Mkoa wa Morogoro unaendesha shughuli zake katika Halmashauri za Ifakara, Ulanga, Kilosa, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Malinyi, lengo ni kutoa misaada ya uwezeshaji huo kwa Halmashauri zote tisa za Mkoa huo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.