Baraza la Madiwani Morogoro latakiwa kubuni vyanzo vya mapato
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro limeshauriwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuifanya Halmashauri hiyo kujiendesha yenyewe badala ya kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu,
Ushauri huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo wakati akizindua Mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo uliofanyika Disemba, 11 mwaka huu katika Makao Makuu ya Halmashauri yaliyoko Mvuha.
Mhandisi Kalobelo amesema, Halmashauri hiyo ina vyanzo vingi vya mapato ambavyo bado havijaibuliwa na una maeneo makubwa na mazuri yaliyoiva kwa uwekezaji, hivyo amewataka Madiwanai watumie fursa hiyo kwa ajili ya kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuifanya Halmashauri hiyo kusonga mbele.
“Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro sio Mvuha peke yake, tunaweza kutumia eneo ambalo ni tayari limekwisha iva kwa uwekezaji. tubuni, tutaishi maisha kana kwamba tuko Manispaa” alisema Mhandisi Kalobelo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo
Amesema eneo lote la ukanda wa Mkambarani na Bwawani ni nzuri kwa uwekezaji na kwamba kinachotakiwa ni nia thabiti, maamuzi na kwamba ana amini Baraza lililoingia madarakani sasa litajikita katika kutafuta njia za kujitegemea kimapato na si kulia lia.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kalobelo amelitaka Baraza hilo la Madiwani kujiepusha na Mabishano yasiyo na tija katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, kwa kuwa amesema mabishano hayo yanaicheleweshea Halmashauri kujiletea maendeleo badala yake amewataka kujikita katika kuwaletea wananchi maendeleo. Mhandisi Kalobelo alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka Madiwani kuanza kazi ya kuwatumikia wananchi kwa kuanza na kutekeleza agizo la Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, la kuhakikisha ifikapo Februari 28 wananfunzi wote wawe madarasani wanasoma wakiwa wamekalia madawati, na kwamba hilo ni agizo la Serikali, halijadiliwi lazima litekelezwe.
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mhe. Innocent Kalogeresi akiwa katika kikao cha Madiwani
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Tale Tale, alishiriki kikamilifu mkutano huo
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bakari Msulwa, amewataka Madiwani wa Halmashashauri hiyo kila mmoja kuainishi shule ambazo zina upungufu wa madawati na wana misitu ili kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri na uongozi wote wa Halmashauri kuomba kibali cha kukata miti katika Wilaya hiyo kwa ajili ya kutengeneza madawati ya wanafunzi ili ifikapo Februari 28 mwakani wanafunzi wote wa shule zilizopo katika Wilaya ya Morogoro wawe katika mazingira mazuri ya kusomea kwa lengo la kutekeleza agizo la Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
kushoto, ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewapongeza Wabunge wa Majimbo ya Morogoro Kusini Mhe. Innocent Kalogeresi na wa jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Tale Tale kwa ushindi walioupata huku akibainisha kuwa mipango yao ambayo wameanza kuipanga ina nia ya kuwaletea maendeleo wananchi wao.
Ruth John ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro, ndiye alikuwa Mwenyekiti wa muda wa Mkutano huo wa kwanza wa Baraza la Madiwani.Hapa Mwenyekiti wa muda Ruth John (kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Halmashaur hiyo moja ya vitendea kazi vyake, joho ambalo huvaliwa rasmi wakati wa vikao vya wahe. Madiwani
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi, ambaye katika Mkutano huo alikuwa ni katibu wa kikao, akitoa miongozo mbalimbali kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mhe. Lucas Lemomo wa kutoka Kata ya Matuli ambaye amechaguliwa kwa kura zaidi ya tisini kukalia kiti hicho, kwa niaba ya Madiwani wenzake ameahidi kuvunja makundi yaliyokuwepo hapo awali ambayo yaliyakuwa yanachelewesha maendeleo ya Halmashauri hiyo huku akiahidi kuyafanyia kazi maagizo ya Katibu Tawala wa Mkoa Morogoro Mhandisi Emmanueli Kalobelo hususan katika suala nzima la kubuni vyanzo vipya vya mapato vya Halmashauri ili kuhakikisha Halmashauri hiyo inajiendesha yenyewe.
MHuyu ndiye wenyekiti mpya wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Mhe. Lucas Lemomo
Maafisa Kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Idara ya Serikali za Mitaa, walishiriki Kikao cha Madiwani katika kuhakikisha kuwa uchaguzi wa Viongozi wa Baraza hilo unafuata Sheria,Taratibu na kanuni. kutoka Kushoto ni Christer Njovu na Marcelin Ndimbwa
Naye Diwani wa Viti Maalum wa Kata ya Bwakila Mhe. Asha Nyakaema alieleza namna kata yake inavyoshirikiana na wananchi wake katika kuendeleza Sekta ya Elimu hususana katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati na vyumba vya madarasa.
Baadhi ya Wahe. Madiwani wakiwa katika Mkutano wao wa kwanza
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.