Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amewahakikishia wananchi wa Gairo Mkoni Morogoro kuwa Serikali itatoa fedha za ujenzi wa mradi wa Chagongwe unaogharimu shilingi Billioni 21.14 na kwamba fedha hizo zitaletwa wakati ili kuhakikisha ujenzi unaanza na unakamilika kwa muda uliopangwa ili wananchi wa Wilaya ya Gairo wapate maji safi na salama.
Mhe. Aweso ametoa kauli hiyo Julai 23, 2024 wakati akishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa ujenzi wa mradi wa Chagongwe ukihusisha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Gairo Mjini na Mkandarasi anayejulikana kama FABEC investment Ltd, mradi huo utatekelezwa kwa kutoa maji kutoka Mto Chagongwe na kuyapeleka Gairo Mjini.
Kiongozi huyo amesema licha ya Nchi kuwa na maeneo mengi ambayo yanachangamoto ya maji lakini fedha hizo zimeletwa Wilayani Gairo ili kupunguza adha ya maji, ambapo amewahakikishia wanagairo kuwa Serikali ya awamu ya sita itatafuta fefha hizo haraka na kumlipa Mkandarasi ili aanze kazi hiyo mapema.
"..Nataka niwahakikishie, leo tumesaini, sio tumesaini ili tuondoke, mkandarasi anatakiwa kupewa kianzio tutabana popote kuhakikisha fedha hii inatoka kwa wakati.." Amesisitiza Mhe. Aweso.
Katika hatua nyingine Mhe. Aweso amepiga marufuku kwa Mamlaka za Maji kuwabambikia bili za maji wananchi ambazo sio sahihi, ambapo amesisitiza kulipa bili ya maji kulingana na mita inavyosoma, pia kushirikiana na mwananchi wa mahali husika pindi msoma mita anapoenda kusoma ili kuepuka udanganyifu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira Gairo Mjini (GUWASA ) Mhandisi. Felister Joseph amesema mradi huo unaogharama Shilingi Bilioni 21.14 unatarajia kukamilika mwaka 2026 na utahudumia wakazi wapatao 156,000 wa Kata 11 za Chagongwe, Rubeho, Msingisi, Gairo, Magoweko, Ukwamani, Mkalama, Chigela, Kibedya, Chakwale na Madege.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.