Mkoa wa Morogoro umeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Kilimo, Mifugo na uvuvi, (2020/2021 hadi 2025/2026) ambapo zao la Mpunga kwa Mkoa huo limekuwa ni zao la kwanza kwa uzalishaji na limewekewa malengo kwenye mpango kuwa na ongezeko katika uzalishaji kutoka tani 905,425 mwaka 2021 kufikia tani 1,489,436 kwa mwaka 2026.
Hayo yamebainisha Novemba 24 mwaka huu na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Warsha ya kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu katika Mnyororo wa thamani wa zao la Mpunga kupitia mradi wa SOUTH – SOUTH AND TRIANGULA COOPERATION (SSTC) uliofanyika katika Ukumbi wa Kings Way katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mhandisi Kalobelo amesema mpango mkakati huo umetokana na zao la Mpunga kuwa zao la pili la chakula Tanzania baada ya Mahindi ambapo idadi kubwa ya wananchi hutegemea zao hilo kwa ajili ya chakula na biashara.
Pia amesema Serikali ya wawamu ya tano ya Mhe. Dkt John Pombe ,Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 13 2020 wakati akifungua bunge la 12 alitaja Kilimo kuwa moja ya kipaumbele katika Serikali kwa miaka mitano ijayo ikilenga kuongeza ufanisi katika tasnia hiyo ili kukifanya kilimo kuwa zao la kibiashara.
Aidha, Mhandisi Kalobelo huyo amesema kuongezeka kwa zao la mpunga kunapelekea kuimalika kwa usalama wa chakula, kuongezeka kwa ajira na kipato kwa wakulima walio wengi hususan wadogo.
Sambamba na hayo, Serikali imeandaa mkakati wa Taifa wa mazao baada ya kuvuna kwa miaka 5 2019/2029 ambao umesambazwa katika Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro na uongozi umeundwa kwa ajili ya kusimamia na kuzuia upotevu wa mazao likiwepo zao la mpunga.
Kwa upande wake Mwakilishi Msaidizi wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Kimataifa (FAO) Charles Tulahi amesema uzalishaji wa mpunga unahitaji usimamizi mzuri kabla na baada ya mavuno na matumizi sahihi ya zana za Kilimo kwa kuzingatia Teknolojia za kisasa.
Akizungumzia changamoto zinazoikumba sekta ya Kilimo cha Mpunga, Tulahi amesema zao hilo linakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ubovu wa miundombinu katika usafirishaji wa zao hilo mara baada ya mavuno.
Amesema changamoto nyingine sekta ya kilimo ni Elimu ndogo waliyonayo Wakulima juu ya upandaji wa zao hilo hali inayopelekea kupungua kwa uzalishaji wa zao hilo la mpunga wakati wa mavuno.
Tanzania ni Nchi ya pili kwa uzalishaji wa zao la mpunga katika bara la Afrika baada ya Madagascar, ambapo Mkoa wa Morogoro ndio Mkoa wa kwanza kwa uzalishaji wa zao hilo hapa nchini.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.